MSIPOONGOKA NA KUWA KAMA VITOTO HAMTAINGIA KATIKA UFALME WA MBINGUNI……….

 

MSIPOONGOKA NA KUWA KAMA VITOTO HAMTAINGIA KATIKA UFALME WA MBINGUNI……….

Na: Min. Mathayo Daudi Sudai

Bwana Yesu asifiwe watu wa Mungu….karibu katika siku nyingine tutazame jambo hili…

Siku moja wanafunzi wa Yesu walikuwa wanabishana juu ya nani aliye mkuu au mkubwa kicheo katika ufalme wa mbinguni na wakaamua kumfuata Mwalimu wao, Yesu kristo ili awape jibu sahihi la hilo swali lao…..

Tusome hapo kidogo

Mathayo 18:1-4
 Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema,  Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.

 

Katika kutoa jibu Yesu alianza kuwapa masharti ya mtu kuingia kwenye huo ufalme wa mbinguni kabla ya kuwapa jibu lao….

Na hapa inatakiwa kila mtu ajifunze kwamba kuyaongelea maswala ya ufalme wa mbinguni kama wewe si muhusika au mtu asiyetaka kuingia kwenye ufalme huo basi ni kupotea muda na kuwa na mazungumzo yasiyo na faida…

Unaweza kuyajua mambo mengi ya ufalme wa mbinguni lakini hayo yote yasikuhusu wewe…..na ndivyo ilivyo kwa watu wengi katika dunia ya leo…..unaweza kukutana na mtu anakuuliza maswali yanayohusu ufalme wa Mungu, lakini ukimwambia habari za kuingia kwenye ufalme huo unakuta hataki tena yupo mbali kabisa na kuona wokovu ni kama kupoteza muda…..sasa yale maarifa anayoyataka unakuta hayamsaidii kitu…..
kumbe inatakiwa tuyajue mambo ya ufalme wa Mungu kwa lengo la kukua na kuongezeka katika mambo ya kimungu au kiroho na si kujua tu huku hakuna hatua tunayoichukua…..

Yesu alipoulizwa akajua kwamba wakibishana kuhusu nani aliye mkuu katika ufalme wa Mungu na huku ufalme huo hauwahusu basi hata jibu atakalowapa halitawasaidia kitu….na ndiyo maana alitoa kwanza njia pekee ya mtu kuingia kweney ufalme wa Mungu na ndipo akawaambia jibu la swali lao…….

“Msipoongoka na kuwa kama vitoto hamtaingia katika ufalme wa MUNGU…….”

Hili ndilo neno la Yesu alipoanza kujibu swali…..
alipoongea kuhusu watoto alikuwa na maana kwamba watu wanatakiwa kugeuka na kuwa kama watoto wadogo si katika umri bali katika mambo fulani kama vile

·        Wasiwe na hatia mbele za Mungu…ili ufae kuingia katika ufalme wa Mungu na kumuona Mungu basi ni lazima usiwe mtu mwenye dhambi bali uwe kama mtoto ambaye yeye huwa hana hatia moyoni mwake, hivyo ili ufae lazima kudumisha utakatifu ambao ndiyo unaokupa ujasiri wa kusimama mbele za Mungu….

 

Mathayo 5:8

Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu”

 

·        Wawe wanyenyekevu……mtoto mdogo ni mtu ambaye hana nguvu mbele ya kila mtu aliye mkubwa wake na mara zote watoto wachanga huongozwa na wazazi wao maana wao hawawezi kujiongoza,…na hivyo ndivyo mtu anatakiwa kuwa mbele za Mungu ili aweze kuingia katika ufalme wa mbinguni…maana bila kukubali kuongozwa na Mungu basi ni lazima tujue kwamba hakuna awezaye kuzaa matunda ambayo Mungu anayahitaji kwa watu wake na kama hawezi kuzaa matunda basi hataweza kuingia katika ufalme wa Mungu bali atakatwa na Mungu mwenyewe na kutupwa nje katika moto

 

Yohana 15:5-6

Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.

 

Hivyo kuingia katika ufalme wa Mungu basi ni lazima ukubali kuongozwa na Mungu mwenyewe mbali na hapo utapotea na kwenda katika njia isiyo sahihi isiyokuingiza katika uzima wa milele

 

·        Wawe na imani…..tunajua kwamba watoto wadogo ni watu ambao huwa wanaamini kwa wepesi kila kitu ambacho huwa wanaambiwa na wazazi wao, au wale wanaowafundisha….sasa ukiongoka na kuw akama mtoto katika nafasi hii maana yake uwe na imani juu ya kile ambacho Mungu anakwambia, tena unapotembea tembea kwa imani, unapotenda au kuomba basi uwe na imani na hiyo ndiyo itakufanya umpendeze Mungu….

 

Waebrania 11:6

 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

 

Kwahiyo ni lazima mtu awe kama mtoto katika kuamini..yaani amini kila ambcho Mungu anakwambia na hapo waweza kuingia katika ufalme wa Mungu…kama Mungu kasema atakubariki basi AMINI, kama kasema atakuwa na wewe na kukulinda basi AMINI…kama ni kuinuliwa basi AMINI….maana yeye Mungu hawezi kudanganya….

Hesabu 23:19

Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

 

·        Wawe na Upendo…..Tunafahamu kwamba mtoto mdogo humpenda kila mto tena hao watoto wachanga ni watu wasiomchukia mtu yeyote…sasa katika kipengele hiki Yesu alilenga kuwaonyesha kwamba wanatakiwa kuwa na upendo kwa watu wote na wasiwe wa kuhifadhi chuki mioyoni mwao…. 


1 Yohana 2:9-11

Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

 

·        Wawe wenye kusamehe…..ukitembea katika dunia hii popote pale hutakuta mtoto mdogo/mchanga akiwa na kisasi na mtu yeyote…mtoto mchanga hata kama ukimfanyia mambo mabaya yeye hakuchukii wala halipi kisasi bali huwa kama mtu aliyeachilia msamaha moja kwa moja maana hajui mambo hayo ndani mwake…..Hivyo Yesu aliposema wawe kama watoto maana yake wawe ni watu wa kusamehe na kuachilia pale ambapo watu watakuwa wamewakosea na hii ni kwasababu kusamehe ni ufunguo wa wewe kusamehewa na Mungu lakini usipokuwa mtu wa kusamehe basi hata Mungu aliye mbinguni hatoweza kukusamehe wewe na dhambi zako…

 

Mathayo 6:14-15

 Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

 

Je wewe mtu wa Mungu unafanana na mtoto mchanga katika maisha yako, kama ndiyo basi endelea kuwa kama kitoto kichanga mbele za Mungu katika tabia hizo zote , lakini kama HAPANA basi ni lazima uongoke/ugeuke leo na kuanza kuzirudia tabia za mtoto mchanga kama neno la Bwana lisemavyo ili tu upate kuwa na nafasi katika ufalme wa mbinguni….

Unapoamua kumgeukia Mungu, kutubu na kumtii yeye kwa matendo basi tambua yeye ni mwaminifu na atakusafisha kabisa na utakuwa na nafasi kwake haijalishi ulitenda dhambi gani, kubali leo na Mungu akusafishe…..lakini ukifanya moyo kuwa mgumu basi kuna hatari mbele yako, UTAANGAMIA…

 

1 Yohana 1:9

Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.

 

MUNGU AKUBARIKI KWA JINA LA YESU.

 

Taifa Teule Ministry
Min. Mathayo Sudai
0744474230/0714732009

 

 


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI