NAFASI YA MUNGU KATIKA MAOMBI/MIPANGO YANGU


NAFASI YA MUNGU KATIKA MAOMBI/MIPANGO YANGU

Bwana Yesu asifiwe watoto wa Mungu 

Karibu katika ujumbe huu👇

👉Katika Maombi / Mahitaji yetu tunayoyaomba kila wakati kwa Mungu, Wakati mwingine kuna mambo ambayo tunayataka na kuyaomba lakini mambo hayo yamebeba kusudi la Mungu pasipo sisi kujua.

Tunaweza kusione mpenyo au majibu mpaka pale tutakapoyaomba katika njia sahihi inayoendana na matarajio ya Mungu katika mambo hayo.

Mfano:

Hanna alitamani kupata mtoto kwa muda mrefu, lakini Alikuwa amefungwa tumbo lake. Kilichomfanya atamani zaidi na wakati mwingine kumuomba Mungu ni kwasababu ya mke mwenzake ambaye alikuwa anamcheka, na kumdhihaki. Si jambo la Kupinga kuwa Hanna alitaka mtoto ili aweze kumfunga mdomo mke mwenzake. 

Pia alitamani amfurahishe mumewe na apate amani katika nyumba yake. 

Lakini vipi kuhusu Mungu? Mungu alikuwa na kusudi juu ya uzao wa Hanna, ukizingatia Eli na watoto wake walishaharibu, Mungu alitaka kuinua kuhani mwingine.

Tunajua Utumishi wa Mungu hauji tu kawaida, mtumishi anaandaliwa hata kabla mimba haijatungwa Mungu ameshachagua watumishi wake katika viuno vya watu. (Yamkini na wewe ni mmoja wapo wa watumishi ambao Mungu amewakusudia kwaajili ya kazi yake. wakati mwingine Unaweza usijitambue kwa Sasa lakini wakati wa Mungu ukifika utaitambua nafasi yako.)

Hana hakulijua hilo, aliomba mtoto kwa manufaa yake ambayo ni kinyume cha Matarajio ya Mungu. Siku alipoomba sawasawa na matarajio ya Mungu ndipo alipopokea majibu ya maombi yake.

1Samweli 1:11

[11] Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.

Yapo mambo unayoomba kwa muda mrefu ambayo yamebeba utukufu wa Mungu,Yapo mambo unayotia bidii kuyafanya lakini huoni mpenyo kwasababu lipo kusudi la Mungu ndani yake.

Unayaomba au kuyafanya ukiwa na matarajio yako binafsi lakini Mungu anashauri lake juu ya Jambo hilo. Shauri la Mungu juu ya jambo hilo ndilo linalosimama ndani mwa mtu, na kwakuwa hujajua lipo shauri la Bwana ndiyo maana shauri lako katika jambo hilo halitimii, ndiyo maana kila ukikazana huoni majibu, ndio maana matarajio yako huoni yakitimia katika jambo hilo Subiri kwasababu majibu ya maombi yako ni mchakato, Bwana atatimiza tu.

Zaburi 33 :10 -11

[10] Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu.
[11] Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.

Hanna aligeuza maombi yake kuelekea mapenzi ya Mungu,  alipata akili ya kujua kuwa vyote vilivyoumbwa ni kwa utukufu wa Mungu, hivyo aliacha kuomba mtoto kwa utukufu wake akaomba kwa utukufu wa Mungu.

Kwakuwa shauri la Bwana ndilo litakalosimama, Mungu akamjibu Hanna, Mungu akampa mtoto mwanamume kama alivyoomba.

Ni vyema sana kuomba mapenzi ya Mungu kwenye kila tunaloliomba, haijalishi ni kubwa au ni dogo,  ni vyema sana kuangalia Mungu anataka nini kwenye kile unachokifanya, ni kwa namna gani kitamrudishia utukufu Mungu na ukifanye kwa namna ambayo kitamrudishia Mungu utukufu.

Ni faida gani Mungu atapata kwenye hiyo biashara yako, ni nini Mungu atafaidika kwa hiyo ndoa yako, watoto wako, kazi yako.Tafuta sana nini mapenzi ya Mungu kwenye kila ukitakacho, Mwambie Mungu na uombe kwa namna alivyoomba Hanna. Kuyatafuta mapenzi yetu katika maombi yetu ni kupoteza Muda, Mungu amefanya kila kitu kwa kusudi lake,hivyo ni vyema kuyatambua makusudi ya Mungu na kuyafanyia kazi.


Mithali 16

[4]Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake;...


Barikiwa Sanađź‘Ź


Taifa Teule Ministry

Mwl Beata Tito Silwimba.

0742442164 /0620507212 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI