UWE MWAMINIFU HATA KUFA
Bwana Yesu asifiwe watu wa Mungu.
Karibu katika wakati mwingine wa kujifunza maneno ya Mungu na leo tutatazama kifungu cha
Ufunuo 2:9-10
Karibu sana......
Soma hapa👇
Ufunuo wa Yohana 2:9-10
[9]Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.
[10]Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.
Leo naomba tutazame kifungu hiki cha Biblia ambacho kanisa la pili liliambiwa.
👉Kipindi hiki ni kipindi ambacho kanisa la Mungu(waliookoka) walikuwa wakipitia kipindi kigumu cha mateso mengi chini ya wafalme kumi
👉Ni kipindi ambacho watu waliabudu kwa taabu sana na ilikuwa si ruhusa kumuabudu Mungu aliye hai bali Rumi walikuwa na miungu yao ambayo waliwataka watu wote waiabudu hiyo na wafalme wengine walitaka kuabudiwa wao.
👉Kanisa la Mungu lilipokuwa likiendelea kuishika kweli ya Mungu, basi lilipitia taabu sana na wengi kuuawa na wengine kuteseka magerezani na wengine kunyanyaswa sana kwa mateso mengi.
Sasa Yohana alipewa ujumbe wa kwenda kuwaambia watu wa Mungu wa kipindi hicho wa kanisa ili kuwatia moyo kwa ugumu wahaokutana nao kwa kuishika kweli.
Kanisa hilo liliitwa smirna ambapo smirna maana yake ni MACHUNGU au tunaweza sema MACHUNGU NDANI YA KANISA.
Ni kipindi ambacho watu walikufa sana kwasababu ya imani.
TUCHUNGUZE VITU VIFUATAVYO
1. Naijua dhiki yako na umaskini wako lakini u tajiri
Hapo unaona Yesu anawaambia kwamba yale yote wanayoyapitia yeye anayaona
👉Kuteswa, kuhukumiwa vifungo, kuaawa hadharani na hata kunyanyaswa kote ambako kanisa la Mungu lilikuwa linapitia, Yesu alikuwa anawaona na si kwamba alikuwa amewaacha!
Aliwaambia anaiona taabu yao na ule umaskini waliouopata kwakuishika kweli lakini wao ni matajiri sana.
Hii ikusaidie kujua kuwa utajiri ulionao ni mkubwa sana zaidi ya ule unaouona kwa macho.
👉Kuna taabu fulani Mungu anaziruhusu ili zifanyike daraja la kukuinua juu
👉Pengine toka umeokoka umeona watu fulani wamekukimbia
👉Pengine ulipookoka ukafukuzwa kazi
👉Pengine ulipookoka ndugu walikukataa
👉Pengine kuna biashara zako zilizoharibika baada ya kuokoka.
👉Pengine wokovu umekufarakanisha na watu fulani wenye vyeo vya dunia hii.
Leo nakwambia USIOGOPE
Mungu anaiona hiyo taabu na huo umaskini wako kwa kuishika kweli ya Mungu lakini wewe ni tajiri sana
Hebu soma hapa👇
Warumi 8:16-17
[16]Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;
[17]na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
Kwasababu wewe ni mtoto wa Mungu, basi ni lazima ujue kuwa kuna kipindi cha kuteswa na kudharauliwa na kukataliwa na kudhihakiwa kama Yesu alivyofanyiwa ili na wewe upate kutukuzwa juu sana kama vile Kristo alivyotukuzwa juu sana.
Na hapa ndipo penye siri ya utajiri tulionao watu wote tunaoongozwa na Roho mtakatifu(Wana wa Mungu) na ndiyo maana inakupasa ushukuru kwa kila jambo maana hata mabaya kwetu sisi yamebeba siri kubwa.
2. Najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.
Akawaambia kuwa anajua na matukano, kashfa na dhihaka zinazotoka kwa watu waliokuwa na vazi la kiyahudi lakini kimsingi hawakuwa wayahudi halisi bali ni vibaraka wa shetani
👉Kulikuwa na watu ambao walijifanya ni wa Mungu, wayahudi na kutumia kivuli cha utumishi wa utume lakini ndani yao na mafundisho yao yaliyokuwa yanalidhihaki jina la Yesu.
Kivipi?
Mfano, katika dunia ya leo kuna watu ambao wanajiita mitume au manabii, lakini ukiwachunguza wanachokifanya na kukihubiri utagundua si mitume wala manabii kama wanavyojiita wao.
👉Sasa kwa yale mafundisho yao, na ushuhuda wao adui anapata nafasi ya kulitukana kanisa la Mungu,.
👉Wanadamu ambao ni adui wa kanisa wataanza kuona kuwa ukristo au kuokoka ni ujinga, kwasababu ya yale mafundisho wanayoyasikia kutoka kwa wale wanaojiita watumishi lakini si watumishi halisi.
👉Kwa vitendo kama hivi vya watumishi feki wa namna hii, basi kanisa la Mungu linakuwa linadhihakiwa, linatukanwa au linakuwa linapokea matukano ambayo kimsingi kwa asili hayatoki kwa watu wa mataifa bali ni kutoka kwa wale ambao wanajifanya watumishi lakini siyo.
Yaani wanalitukanisha jina la YESU.
Na watu kama hao walikuwepo katika kipindi hicho kama vile walivyo kwenye kipindi hiki.
👉Kuna wengi wamebaki kujiita wakristo lakini maisha yao yanalitukana jina la YESU.
👉Wameharibu ushuhuda na kukosa adabu mbele za wanadamu na Mungu.
Na watu hao adhabu yao imeshaandaliwa tayari na wataipata kama wasipotubu maana Kristo anasema atawakataa japo wao wanajiita wakristo.
Soma hapa👇
Ufunuo wa Yohana 3:15-16
[15]Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
[16]Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
Kuwa makini usiwe kwenye kundi hilo na kama upo, fanya haraka utoke kabla saa ya kupata ujira haijawadia.
Soma hapa👇
Ufunuo wa Yohana 3:1-2,15-16
...... . Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.
[2]Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu.
3. Usiogope mambo yatakayokupata
kanisa lilikuwa linateseka kwa kuishika njia ya haki, lakini Yesu akawaambia wasiogope kwa yale yatakayowapata.
Kumbuka Mungu anajua kila kitu maana yote ameyaruhusu yeye kwa kusudi lake mwenyewe.
👉Anapokwambia usiogope, anauhakika kwamba kwa chochote kitakachokupata, yeye atakulinda na kukuhifadhi.
👉Anapokwambia usiogope anajua mwanzo wa vita yako na mwisho wake ila anakutaka wewe tu usimruhusu shetani kushinda maana hofu si hali bali ni roho mchafu.
👉Lazima ujue kuwa popote palipo na hofu, hapana Mungu na ndiyo maana Biblia imesema USIOGOPE mara 50.
Mungu anajua kila kitu, yaani uzuri unaopitia na ubaya wote yeye anaujua na leo anakwambia usiogope.
Akasema, usiogope mambo yatakayokupata, akiwa na maana kuwa mpango mzima wa shetani alikuwa anaujua na anaona kila alichokipanga shetani kwa ajili ya kanisa. Lakini akasema USIOGOPE kwa chochote ambacho shetani atakileta kwako.
Kwanini?
Yeremia 29:11-12
[11]Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
[12]Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.
Hata kama hali mbaya inaonekana kwenye maisha yako sehemu yoyote ile basi ni lazima uwe na hekima ya kukumbuka kwamba kuna mawazo fulani Mungu anakuwazia.
Lakini je ni mawazo gani?
"Mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho"
4. Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi.
Unajua siku zote lazima Watu waliookoka wawe na macho ya kutazama na hekima ya kulichambua tatizo au changamoto pale inapowapata.
👉Unapopata tatizo usikimbilie kwenye kipengele cha kusema.... Mungu mbona kama hunioni?
👉Unapopata shida usikimbilie kumkukuru Mungu, kama alivyofanya mke wa Ayubu(rejea somo)
👉Unapoingia kwenye taabu usiwe na roho ya uvivu ya kukata taama.
Kwanini?
Kwasababu kuna matatizo, shida na taabu zingine zinaletwa kwako kwa mkono wa shetani na Mungu anaziruhusu ili ujaribiwe.
👉Kwamba je umeokoka kweli au wokovu wa kipindi cha raha tu?
Kuna nyakati zinakuja ili kuwadhihirisha walio wa Mungu halisi, ambao wao liwe giza iwe nuru hawawezi kumkana Mungu.
Shetani anaweza akakupiga kwa ugonjwa au umaskini kwa lengo la kukujaribu tu kama alivyomfanyia Ayubu.
Na hata hawa wa kanisa la pili, walifanyiwa hivyo, baadhi yao walinyongwa, wengine wakatupwa gerezani na wengine kuchomwa mkuki hadharani, kwasababu shetani alilenga kuwajaribu kanisa la Mungu.
Hebu jiulize🙇♀️
Leo hii ikitoka amri kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kumwabudu Mungu, na atakaye abudu anauawa au anafukuzwa kazi.
Na wakati mwingine unaweza kuona kabisa waliokiuka wanafanyiwa hivyo yaani kuuawa au kufukuzwa kazi
Je wewe utafanyaje,?
sasa hapo jiulize, lakini ukishajiuliza usijibu kwa sauti bali sikiliza sauti ya ndani.
Ukiona,
👉sauti inakwambia kwamba kazi yenyewe ulipata kwa taabu halafu leo uipoteze?
👉Sauti inakwambia nikifukuzwa kazi nakula wapi?
👉Sauti inakuambia kufa hapana bora niache kuabudu,
Basi ni lazima ujue kuwa misuli yako ya imani ni midogo sana na unahitaji msaada.
Anayemwamini Mungu na mwenye misuli ya imani, atasikia sauti inamwambia NIKO TAYARI KUACHA VYOTE NA KUMFUATA BWANA. Halleluyaaa!!!
Hebu soma hapa👇
Luka 14:26
[26]Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Hapa si kumchukia chuki ya kimwili kama muuaji bali kuwa tayari kuwaacha na kujikana mwenyewe kwaajili ya Yesu.
Yaani
👉Uwe tayari kuwaacha wao au kwa ajili ya kuambatana na Yesu.
👉Uwe tayari kuachana na mila za wazazi za asili kwaajili ya kuwa na mila za mbinguni
👉Uwe tayari kuacha biashara zako haramu ili uwe na Kristo
Na ndiyo maana aliyeokoka
👉kukataliwa na watu wa dunia hii ni kawaida tu
👉Kutengwa na jamii kwa ajili ya wokovu ni kawaida
Kwasababu undugu wa mwilini ni wa muda tu bali undugu wetu ni katika kristo na ndipo umoja wetu wa kudumu ulipo.
Yesu mwenyewe alisema hayo, hebu soma hapa👇
Luka 8:19-21
[19]Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano.
[20]Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe.
[21]Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
5.Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.
👉Hata kama utanyanyaswa kiasi gani,
👉Hata kama utatengwa na nani,
👉Hata kama utakosa watu wa kukusaidia na kukufariji,
👉Hata kama utafungwa gerezani,
👉Hata kama utaambiwa huruhusiwi kuuza na kununua,
👉Hata kama utaambiwa huruhusiwi kufanya biashara yoyote
Ikiwa hayo yote yatakuja kwako kwasababu ya imani na kumwabudu Mungu, basi usithubutu kumkana Yesu hadharani namna hiyo.
Kwasababu Yesu alisema👇
Luka 12:8-9
[8]Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu;
[9]na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
Na ukiweza kumshinda shetani na kuendelea kumwabudu Mungu bila kujali sababu basi ameahidi atakutukuza na kukuheshimisha mbele za malaika wake wote.
Je umeokoka? Kama bado, basi huu ni wasaa mzuri sana wa wewe kumpokea Kristo ili uiepuke adhabu ya waovu wote iliyoandaliwa kwa saa ya Mwisho.
Kwa msaada ya kuokoka na kubatizwa ubatizo sahihi basi piga kwa namba hizo chini👇 kwa mawasiliano,
Na Mungu akubariki sana
Taifa Teule Ministry
Mwl / Ev Mathayo Sudai
0744474230 / 0628187291
WhatasApp no: 0628187291
Maoni
Chapisha Maoni