NAFASI YA MKE KATIKA KUHARIBU NDOA YAKE



 NAFASI YA MKE KATIKA KUHARIBU NDOA YAKE

Bwana Yesu asifiwe mabinti wa Kristo leo naomba kukujulisha kuhusu jambo fupi sana ambalo limekuwa ni tatizo kwenye ndoa nyingi, bila kujua kwamba Biblia imetoa mwongozo mzuri tu kwa namna ya kuishi baina ya mke na mume.

Tusome hapa👇

Waefeso 5:25-26
[25]Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;
[26]ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;

Ukisoma vizuri Biblia utagundua mbali na mambo yote ndani ya ndoa, mwanaume ameambiwa jambo moja la msingi ambalo Mungu alimaanisha kitu fulani ndani yake.

Jambo lenyewe ni WAPENDENI WAKE ZENU.

sasa unaweza usielewe kwanini Mungu alimwambia hivi mwanaume.

Kwa asili Mungu alipomuumba mwanamke, alimpa asili ya kitu kinachoitwa MWITIKIO.

Sasa huu mwitikio unategemea sana kutoka kwa mume wake, yaani ni kwamba mwanamke ameumbwa kama mtu mwenye sifa ya👇

👉Kuitikia maono yanayotoka kwa mume
👉Kuitikia upendo kutokana na upendo wa mume
👉Kuitikia tabia kulingana na tabia za mume
👉Kuitikia hamasa kulingana na anavyohamasishwa na mumewe

Na ndiyo maana, ili kujua tabia za mwanaume inakufaa sana umchunguze mkewe maana mke huwa anaishi kulingana na mwongozo wa mume.
 
👉Mume akiwa mchoyo, hata kama ataigiza kuwa si mchoyo lakini tabia yake itaonekana kwa mkewe.
👉Mume akiwa na upendo wa dhati kwa mkewe hata asiposema, upendo wake utaonekana kwa mkewe.

Yaani mke amefanywa kuwa kioo cha mume.

Mungu kusema mume ampende mkewe alijua kabisa kuwa, mume akimpenda mkewe basi na mke atampenda sawasawa na upendo aliompenda yeye.
  Na ndiyo maana baada ya pale Mungu hakumwambia tena mwanamke ampende mumewe.

Bali alimwambia mke amtii mumewe na hapa ndipo penye shida kwa wanawake wengi. 👇

Wakolosai 3:18
[18]Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.

Kama Mume anampenda na kumuheshimu mkewe mambo yote yanakuwa yamekamilika kwa asilimia 50% na hizi hamsini zilizobaki zinakutegemea wewe mwanamke ili kuimarisha ndoa yenu.

Wewe binti ni lazima ujue katika ndoa yako utakayoingia unatakiwa ukamilishe deni la asilimia 50% kabla ya mambo yote na mipango yote

Lakini hata kama mume atakupenda, usipokuwa na utii kwake basi jua kuna tatizo kubwa sana bado.

  Kuna maajabu mengi sana kwenye dunia ya leo ambapo tunaona wanawake wengi mitandaoni na kwenye mazingira yetu ambao kwa namna wanavyoishi wanatupa kufahamu kwamba wameacha agizo la Mungu kabisa.

Kimsingi, mwanamke mwenye kumtii mumewe

👉Hawezi kumvua nguo mumewe hadharani kama wanawake wengi wapumbavu wanavyofanya kwenye maisha ya leo.
  Yaani mwanamke anaona ni kawaida kabisa kwenda kwenye vyombo vya habari na kumdharirisha mumewe.

👉Hawezi kukaa na marafiki zake na kutoa siri za ndani za mumewe.
👉Huwezi kuwa na uwezo wa kuungana na adui na kumshambulia mumewe.

   Kwasababu huo siyo mwitikio ambao Mungu aliuweka ndani ya mwanamke.

Binti ambaye unajiandaa kuingia kwenye ndoa jitahidi sana kujua mume anayetakiwa kukuoa ili kwamba utakapoolewa naye, uwe na uwezo wa kuitikia sawasawa na mapenzi ya Mungu.

Usiwe kama wanawake ambao hawaoni shida kuachana na mume mmoja na kuolewa na mwingine
Usiwe kama mmoja wa wanawake wapumbavu akiowasemea mtumishi wa Mungu Ayubu alipokuwa anamjibu mkewe.

Ni lazima ujue kumtii yule ambaye utakubali awe kichwa cha familia yako.

Kumbuka 
👉kichwa cha familia ni mumeo si wewe.
👉Baba wa familia ni mumeo si wewe

Mambo anayoyapanga basi wewe una jukumu la kutii katika Bwana, na pale unapoona uamuzi hauko vizuri basi ni lazima ukumbuke kuwa wewe ni msaidizi wa mumeo inakupasa utimize jukumu lako la MSHAURI NDANI YA NDOA. 

Hata kama mume wako amekengeuka, usijaribu kuonyesha dhahiri kwamba humtii bali fanya hivi👇

1 Petro 3:1
[1]Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;

Endelea kuonyesha na kujionyesha kwake kuwa wewe ni msaidizi wake, na kana kwamba hujui chochote zaidi yake, huku ukiishi naye kwa hekima na upole ili kwa mwenendo wako mzuri basi umvute na kurudi katika njia salama. Na Mungu atakuinua sana nawe utakuwa mke bora. 

Lakini ukifanya kana kwamba wewe ni mjuaji kuliko yeye basi jua hakuna mume yeyote anayependa kuwa chini ya mkewe kwa asili kabisa. 
  Bali hupenda kupata ushauri tu kutoka kwa msaidizi wake yaani mkewe. 

Hebu soma hapa👇

Mithali 14:1
[1]Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; 
Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

Mwanamke mwenye hekima si mjinga, si mtu wa kelele mabarabarani na kwa marafiki zake kuhusu shida za nyumbani mwake. 

Soma hapa👇

Mithali 9:13-15
[13]Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, 
Ni mjinga, hajui kitu.
[14]Hukaa mlangoni pa nyumba yake, 
Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,
[15]Apate kuwaita wapitao njiani, 
Waendao moja kwa moja katika njia zao.

Hiki ni kipengele cha muhimu sana cha kuilinda ndoa yako, na ndoa yako haitavunjika kamwe. 

👉Ukilijua hilo na kuliishi basi wanawake wengi watakuja kwako na wewe utakuwa mshauri wao. 

Nafasi ya mwanaume katika familia ni hii
👉Kichwa, Mume, na Baba

Nafasi ya mwanamke katika familia ni hii
👉Malkia, mke na mama

   Nafasi hizi tatu kwa watu wote zimebeba majukumu fulani ambayo kila mtu anatakiwa kuyatimiza sawasawa na nafasi yake. 

Ukiwa mke mtii, mpole, mwenye hofu ya Mungu basi wewe ni moja ya wanawake wa kibiblia. 

Ni matumaini yangu kuwa utakuwa mmoja wa wanawake wenye sifa zao za asili walizopewa n@a Mungu pale Edeni. 

Na Mungu akubariki sana



Taifa Teule Ministry 
Mwl / Ev Mathayo Sudai 
0744474230 / 0628187291 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI