MISINGI 10 YA NDOA ISIYOVUNJIKA
MISINGI 10 YA NDOA ISIYOVUNJIKA
Bwana Yesu asifiwe mabinti wa kristo
Leo naomba kuwashirikisha misingi au Sheria10 zitakazofanya ndoa yako kuwa ndoa imara isiyokuwa na tatizo kati yenu wawili mke na mume.
Hebu soma hapa kwa makini na utaratibu maana ndipo penye misingi hiyo
Mwanzo 2:18-25
[18]BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.
[19]BWANA Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake.
[20]Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye.
[21]BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,
[22]na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.
[23]Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.
[24]Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
[25]Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.
Naomba Mungu akutie nguvu kuusoma ujumbe huu uliondaliwa na ndugu yako Mwl/Ev Mathayo Sudai kwa lengo la kukufikisha ng'ambo kwa jina la Yesu.
Karibu sana.....
Hapa ni misingi kumi ya kibiblia, ambayo inaweza ikakushangaza kwasababu si ya hekima ya dunia inayoshikiliwa na watu wengi ila hii ni ya Mungu mwenyewe na ndiyo ifanyayo ndoa kuwa na furaha na amani katika mpango wa Mungu.
Kumbuka mtu anaponunua gari au kifaa cha umeme huwa anapewa na kitabu cha mwongozo wa jinsi ya kuendesha( kuoperate) ipasavyo na mtu asipofuata mwongozo huo kinachotokea ni
1. Kifaa kutokufanya kazi
2.kifaa kufanya kazi kwa muda mfupi na baadae kufa kabisa.
Sasa ndoa ni kitu alichokifanya Mungu mwenyewe, na pia akaweka mwongozo wa jinsi ya kutembea ili kudumu, na ni hivyohivyo mwongozo huo usipofuatwa basi ndoa hii
1.haitaishiwa migogoro
2.itaishia kwenye taraka na anguko la kiroho
MISINGI 10 YA NDOA ISIYOFUNJIKA NA ISIYO NA MIGOGORO.
Kwana naomba nikusaidie kukujulisha kitu kwamba.
Ndoa bila migogoro inawezekana kabisa, yaani siyo lazima watu wagombane eti ndo iitwe ndoa, hapana!
Tunaweza kuishi ndani ya ndoa kwa amani na upendo kila siku endapo tutafuata misingi hii👇
1.KUSHIRIKIANA KWA VYOTE
Watu wengi wanakosea pale wanapodhani kushirikiana ni kwenye kitanda tu, pale wanaposhiriki tendo la ndoa tu jambo ambalo ni uongo mkubwa wa shetani. Lakini ushirika lazima uwepo kimawao, kushirikishana idea mbalimbali, kushikiana maono ya familia, na kila mmoja lazima amshirikishe mwenzake si mume tu au mke tu ndio amshirikishe mwenzake bali wote tena kwa uwazi kabisa.
Kumbuka kukosa mawasiliano mazuri katika ndoa ni njia pana ya kuwapeleka kwenye talaka.
"nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye."
2. MACHO YAKO KILA SIKU YAANGALIE MAMBO AU TABIA CHANYA ZA MWENZAKO
Kulingana na 1 Wakorintho 13 tunaona kuwa
Upendo unavumilia
Upendo unalinda
Upendo huficha udhaifu/unastahimili
Upendo una adabu
Upendo hauhesabu mabaya ya mwenzako
Ukitaka upendo usipungue katika ndoa yako basi usiwe mtu wa kuangalia madhaifu ya mwenzako kwasababu madhaifu yake ukiyaangalia sana shetani shetani ataanza kukwambia mambo yafuatayo👇
Ivi kwake niliona nini
Ivi kwanini nilimuoa au kuolewa na huyu
Unaweza ukashangaa kila unachokiangalia kwake unakiona kina kasoro na hakikufai na mwisho wake unaanza kutamani nje.
Lakini wewe inabidi uangalie mazuri aliyobarikiwa na Mungu tu, mtazame Kristo aliyekaa ndani yake, ndipo utashangaa ghafla huoni udhaifu wowote kwake, unaanza kumuona yeye ni mzuri kuliko wote, unaanza kuona amekamilika kabisa na anakufaa,
Lakini kwanini kwasababu unampenda na huangalii udhaifu wake ndipo ghafla linatimia neno lile kwamba UPENDO HUFUNIKA VYOTE.
Na ndiyo maana unaeweza kukutana na mtu kaoa au kuolewa ukaanza kujiuliza yule mwenzake alimpendea nini na hadi leo wanaishi pamoja lakini jibu ni hilo juu.
3. MUME HAJAUMBWA KAMA MKE ILA WANAFANANA
"nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye."
Unajua kina maneno mawili tofauti hapa
KUFANANA na KUWA SAWA
COMPARABLE and BE THE SAME
Sasa mwanaume ameumbwa tofauti na mwanamke katika maumbile ya nje, waliumbwa wakati tofauti hawako sawa katika kufikiri, pengine hata katika uwezo lakini mke na mume WANAFANANA,
kumbuka nimesema MKE na MUME sijasema MWANAMKE na MWANAUME
Wanafanana kwamba wameumbwa kila mtu anaweza kumkamilisha mwenzake.
Mfano
Ukichukua karatasi mbili, moja ukamchora mwanamke na nyingine mwanaume,
Ile ya mwanamke itoboe matundu matundu kifuani na ile ya mwanaume itoboe matundu miguuni na nikononi.
Zile picha mbili ukizikata vizuri na kuzibandika pamoja kwa gundi imara, kitakachotokea ni kwamba hautaona tundu hata moja.
Kwanini? Ni kwasababu walikuwa wawili tofauti lakini walivyokuwa pamoja kila mmoja akamkamilisha mwenzake na kufanana. Na hiyo gundi ni upendo wa kimungu kati yao.
4.MSIRUHUSU KUINGILIWA NA WAZAZI WENU
Soma hapa👇
[24]Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
Mnapooana wawili ni lazima kitiu chochote kipangwe na ninyi wawili, siyo kuwaruhusu watu wengine kuingilia maono yenu,
Biblia inaposema ATAMWACHA BABA YAKE NA MAMA YAKE, inamaanisha huyu mtu anaanza maisha mapya kabisa na mtu mpya kabisa na mipango mipya kabisa, yaani ni hivi👇
Kama ulikuwa unashirikiana na wazazi wako kutafuta maisha mazuri, unaacha na unaanza kushirikiana na mume au mkeo
Kama ulikuwa unakaa na wazazi wako kupanga mioango ya kibiashara, unaacha na unaanza kupanga na mwenza wako
Kama ulikuwa una marafiki wa karibu unaowashirikisha maono yako, basi unaacha na kuanza kumshirikisha mwenza kwanza kabla ya mtu yeyote.
Kwasababu mara nyingi tumejua kuna ndoa ambazo unamkuta mwanamke anashirikiana na mama yake mzazi kumfanyia vituko mumewe,.
Yani mke anaacha kushirikiana na mumewe eti anashirikiana na mama yake mzazi na wakati mwingine utakuta kila mume wake akimuuliza kitu anasingizia mama, hiki mbona kiko hivi, anajibu mama kasema hivi na vile. Yani kama unajua unaweza kuwa mke wa hivo basi sahau kudumu kwenye ndoa utaachika tena mapema sana m.
Lakini mimi nakupa siri leo anza kila kitu na mumeo kabla ya wengine
Yaani pointi ya muhimu ni kwamba watu wa nje watahusika katika maisha na mipango yenu pale tu mtakapo waalika nyie, lakini mbali na hapo, ni wewe na mwenza tu kwasababu mwenza wako ni wewe mwenyewe na ndiyo maana ya kuwa mwili mmoja ikiwa na maana kuwa ukimuona mwenza wako basi ni sawa na kujiona wewe mwenyewe.
Kuna watu wengibleo hii unakuta anampango fulani wa maisha, eti anamwacha mwenza wake halafu anaenda kuwashirikisha marafiki au wazazi wake na wala mke wake au mume wake hajui. NI HATARI. Ukiona unafanya hivyo basi tambua hujaambatana bado na mwenza wako.
Kuachana na wazazi maana yake ni kuifanya sektavya ndoa yako kuwa ya kwanza kabla ya vyote
5.IFANYE NDOA KUWA YA KWANZA NA YA KIPEKEE NA USIRUHUSU KITU KIINGIE KATIKATI YENU
Ni lazima ujue umetoka kwenye majukumu ya nyumbani kwenu kabisa kwa wazazi wenu na sasaivi umeingia kwenye msimu mpya ambao mwamuzi ni wewe kama unataka msimu huu udumu au uishe.
Ndoa yako ni lazima uipende, yaani penda kuwa na familia yako, penda kukaa wewe na mumeo au mkeo pengine kama mtakuwa tayari na watoto, basi ni lazima upende kuwa na familia yakovkwa pamoja hata wakati mwingine kufurahi na kucheka, kutaniana taniana kidogo, kufurahi pamoja na vitu kama ivo.
Huwezi kuwa siriazi muda wote umekunja tu sura, ni lazima upate muda kufurahi na mwenzako na watoto kama wapo
Na ni lazima usiruhusu vitu vyenye matokeo hasi au vitu vinavyoweza kuhatarisha ndoa yako na hakikisha haviingii ndani ya ndoa
Mfano.
👉Ondoa kila marafiki wanaoweza kuhatarisha ndoa yako, ambao pengine ulikuwa nao zamani. Lakini ukiona wanaweza hatarisha ndoa yako basi waondoe na tafuta marafiki wapya kwa afya ya ndoa yako
👉Pengine kuna michezo na starehe za aina fulani ulikuwa unazipenda, lakini kama mwezako hazipendi na unaona inaweza kuwa hatari kwa ndoa yako, basi iondoe na tafuta kitu kingine mnachoweza kukipenda wote ili muwe mnafurahia kwa pamoja.
Yaani pointi ni kwamba usijaribu kuingiza kitu ndani ya familia ambacho kinahatarisha ndoa yenu.
Unaweza kuuliza, sasa kama mimi napenda kuabudu yeye hataki si naweza kuhatarisha ndoa yangu, kwahiyo niache kuabudu?
Jibu ni kwamba hukufuata mwongozo wa jinsi ya kuoperate ndoa uliotengenezwa na Mungu pale alipoifanya ndoa na huu ni mwongozo wa nuru kutokufungamana na giza, yaani umeokoka halafu ukaolewa na mpagani,
Yaani ni sawa na kuwa nuruni na kuamua kwenda gizani, na baada ya kuingia gizani ukaanza kumuita Mungu aliye nuruni ukitegemea mwongozo wake utafanya kazi..... Hapo unakua umeshapotea tangu ulivyoanza kucheza mchezo maana yake ulishafeli tayari.
Ni sawa na kuulewa mwongozo wa kutumia gari lakini kabla hujaanza kuendesha gari ukaweka mafuta sehemu ya na maji sehemu ya mafuta. Hata kama utaingiza gia vizuri na kuona mbele vizuri usitegemee kuwa gari litatembea kwasababu ilishakosea mapema.
6. UNGANA NA MWENZA WAKO NA INGIA KWA MIGUU YOTE KWENYE MAJUKUMU YA KINDOA
Soma kipengele hiki👇
"nao watakuwa mwili mmoja."
Kuungana ni neno lenye msingi wa kiebrania ambalo kwa lugha ya kiingereza ni join, au cleave which means adhere - glue
Kwa kiswahili ni kushikamana kwa mithili ya gundi
Chukulia mfano, una vipande viwili vya karatasi nyeupe, halafu ukavipaka gundi kila kipande na kisha ukaviunganisha vizuri na kisha vikakauka kabisa.
Ukija wakati mwingine na kutaka kuviachanisha🙂, unajua nini kitatokea?
Ni kwamba havita achana vizuri bali vitachanikachanika vibaya na kupoteza maana.
Basi hivyo ndivyo wanandoa💕 walivyo na ndiyo maana Mungu akasema kwamba anachukuia watu kuachana kwasababu wakishaachana wanapunguza uhalisia wao, wakinidhani na kiheshima mbele za Mungu
Malaki 2:16
[16]Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.
Pia ni lazima kila mtu katika ndoa aingie kutenda majukumu yake ndani ya familia kwa ustawi wa familia na watoto wake.
Usijaribu kufanya kazi kwaajili ya wazazi wako uliowaacha kwenu kabla ya familia yako,
👉Ni lazima ujue kuifanya nyumba yako imara kabla ya nyumba zingine na kila mtu awe na lengo la kuimarisha ndoa maana hakuna kitu kingine katika mfumo wa maisha baada ya ndoa zaidi ya kifo, kwahiyo fanya majukumu yako kwa bidii kuimarisha familia yako.
7. TALAKA SIYO CHAGUO KATIKA NDOA
Yaani unapoingia kwenye ndoa ni lazima uwe na akiri ya kutambua kuwa hutafunga ndoa nyingine tena iliyo takatifu kama hiyo mpaka labda mmoja wenu afe, 😦
Sasa kwenye maisha ya ndoa ni lazima uepuke sana wazo la kuja kumtamkia mwenzio maneno kama vile "TUACHANE"
Vuta kabisa wazo la kwamba siku moja utakuja kuwa na mwenza mwingine chini ya ndoa takatifu zaidi ya hiyo utakayokuwa nayo. Kwa mantiki hiyo ni lazima ujue jinsi ya kutulia na kumpata mwenza wa kufanana na wewe ukijua kuwa hutoolewa tena au hutooa tena kama ni mwanaume.
Si kila tatizo linaloingia ndani ya ndoa jibu lake ni talaka.
👉Ukiona una mchumba halafu likatokea tatizo kidogo tu na ghafla akakwambia TUACHANE basi ni lazima ujue huyo mchumba akili yake haijakomaa na haitoshi kuwa na familia..... Kuwa makini hapo😯
Matatizo mengine yanakuja yakiwa yameruhusiwa na Mungu mwenyewe, sasa kama mchumba wako anakimbilia kwenye kuachana jua kabisa anaweza asikufikishe pale palipoandaliwa na Mungu, pale panapohitaji uvumilivu mkubwa.
Hebu mkumbuke AYUBU NA MKEWE
Ni Mungu aliyemruhusu shetani amjaribu ayubu, kwa kumletea matatizo, lakini mkewe akachoka ghafla nz kumwambia Ayubu amkufuru Mungu ili afe, 🙆♀️
Yani siri ya pale ni kwamba mke wa Ayubu alitaka mumewe awe na hali nzuri tu kila siku, na kumwambia maneno yale. Kingine ni kwamba alimchoka mumewe ghafla kwa yale matatizo akaona ni bora afe tu, kwa tafsiri nyingine bora TUACHANE TU milele.
Lakini unaona baadae yule mke alikufa kwasababu Mungu alikuwa anampeleka Ayubu kwenye kiwango kingine kikubwa na mkewe hakuwa na nguvu ya kubeba kile alichokuwa nacho Ayubu, hivyo safari ya mke mpumbavu kama mke wa Ayubu iliishia pale., na Ayubu akaendelea kusonga mbele.
Usisubutu kutaka kumkimbia mwenza wako pale yanapokuja matatizo, mengine yameruhusiwa na Mungu kumpeleka mtu sehemu nyingine kubwa zaidi.
8. UFANYE UPENDO UISHI KWENYE NDOA MWANZO HADI MWISHO
Kuna vitu vya ajabu ajabu ambavyo ulimwengu unaviita upendo lakini kimsingi si upendo.
👉Ukiona mtu anakupenda pale unapovaa nguo nzuri na kupendeza, basi tambua kuwa huo sio upendo japo dunia inauita upendo
👉 Ukiona mtu anakupenda kwasababu una pesa kuliko yeye, basi tambua huo sio upendo
👉Ukiona mtu anakupenda kwasababu una rangi nzuri au makalio mazuri au shape nzuri, basi shtuka, huo si upendo japo dunia inauita upendo
Wengi sana katika dunia hii wameoa na kuolewa kwasababu kuna vitu waliviaangalia, mwisho wa siku wameishia kwenye kilio cha ajabu na kuhangaika kuomba ushauri.
Soma hapa👇
Wakolosai 3:14
[14]Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.
Biblia inasema upendo ndiyo kifungo cha ukamilifu
Love is a bond of perfection
Yaani maneno yasiwe mengi ndani ya ndoa, wewe ukitaka kuishi kwa amani na utulivu bila mashaka na kwa ukamilifu wa kimungu basi mpende kwa dhati mwenza wako katika nyakati zote, acha kuishi kama wahuni wa dunia hii ambao akiona mkewe amezaa anawaza kupata mwingine mdogomdogo.
Akiona mumewe hana pesa, anawaza kutafuta mume nje, huo ni upotevu kabisa.
Ulivyokuwa unampenda mweza wako wakatibwa uchumba na ile siku ya kufunga ndoa basi mpende hivyohivyo hata kama watu watasema hana sifa.
👉Usiruhusu watu wa dunia hii wakakwambia sifa mbaya za mwenza wako bali wewe mwenyewe hakikisha inatoka sauti ndani ya moyo wako ya kuwa unampenda, ukiwa hivyo basi sauti za maadui zitakuwa ni kelele na uchafu.
Tahadhari, Hakikisha upendo wako upo katika BWANA, usiseme unampenda tu, bila kuwa ndani ya Kristo.
9. TENDO LA NDOA LIWEPO NDANI YA NDOA
Biblia imezungumza kuhusu uhusiano wa kimapenzi ndani ya ndoa.
Na tendo la ndoa nje ya ndoa ni dhambi
Hebu Soma hapa👇
1 Wakorintho 6:9-10
[9]Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
[10]wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.
Katika ndoa takatifu Biblia inaweka wazi kwamba tendobla ndoa nibla msingi na kila mtu ni lazima alifahamu hilo, na pia ajue kuwa hana amri juu ya mwili wake na hapaswi kumkataza mwenzako tendo la ndoa isipokuwa wawe na kiasi kwaajili ya utukufu wa Mungu na kwaajili ya kufanya ibada.
Kwa mfano kuna siku mnaweza kuwa mmefunga kwaajili ya kufanya maombi ya kitu fulani, sasa katika nafasi hiyo si vizuri kushiriki tendo la ndoa maana mtakosa utulivu wa kiroho na maombi.
Hebu soma hapa👇
1 Wakorintho 7:3-5
[3]Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake[
4]Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.
[5]Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
Usije kuwa umeokoka leo halafu ukaingia kwenye ndoa na kufikiri tendo la ndoa ni dhambi, ukaanza kumnyima mwenzako,..... Hapana✋
Tendo la ndoa ni dhambi likifanyika nje ya ndoa, lakini ni takatifu na linampendeza Mungu likifanyika ndani ya ndoa.
Na tendo la ndoa lina majukumu mawili tu kibiblia ambayo ni👇
1. Kuwapata watoto
2. Kufurahi
Soma hapa uone👇
Mithali 5:18-19
[18]Chemchemi yako ibarikiwe;
Nawe umfurahie mke wa ujana wako.
[19]Ni ayala apendaye na paa apendezaye;
Maziwa yake yakutoshe sikuzote;
Na kwa upendo wake ushangilie daima.
Na hapo Biblia inaonyesha kuwa katika mahusiano, mwenza wako pekeake akutoshe,
hii ni tofauti kabisa na mfumo wa dunia ambao mtu anakuwa na mke wake lakini tena unakuta na mahawala wengine ambao Biblia inawaita ni malaya
Mithali 5:20-21
[20]Mwanangu! Mbona unashangilia malaya, Na kukikumbatia kifua cha mgeni?
Kwahiyo tendo la ndoa ni wewe na mwenza wako tu, akiongezeka mwingine ni shetani.
10. MSHIKAMANISHWE NA UPENDO WA KRISTO KATIKATI YENU.
Kumbuka ndoa ni taasisi ya kwanza ulimwenguni kuumbwa baada ya Mungu kumuumba mwanadamu.
Kwahiyo huu ni mpango wa Mungu kabisa
Na watu wanapoona katika ndoa takatifu ni lazima ujue kuwa si wao tu, bali ni mkono wa Mungu ndiyo uliowaleta kuwa pamoja, baada ya Mungu kuona na kusema👇
"Si vyema mtu awe peke yake"
Na kama ni Mungu mwenyewe basi amemwaga upendo wake katikati yenu hivyo huu upendobwa Mungu ndiyo lazima uwe gundi iliyowashika ninyi wawili.
Kile Mungu atakachokifanya basi muwe tayari kukifanya kwasababu anawawazia yaliyo mema na wala hapendi mteseke.
Soma hapa👇
Maombolezo 3:31-33
[31]Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu
Hata milele.
[32]Maana ajapomhuzunisha atamrehemu,
Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.
[33]Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu.
Wala kuwahuzunisha.
Pia soma hapa uyajue mawazo ya Mungu 👇
Yeremia 29:11-12
[11]Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
[12]Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.
Mungu anawapenda na ninyi hakikisheni mnapendana kwa pendo Kristo lisilojali kasoro, huku mkijua kuwa Mungu yupo pamoja na ninyi katika ndoa yenu.
TAHADHRI
Watu wengi wanaharibiwa katika ndoa zao kwasababu wanajifunza maswala ya ndoa kupitia kuangalia movie mbalimbali zenye visa ya kimapenzi na kindoa na wengine wanajifunza ndoa kwa kusoma magazeti yalioandikwa na watu wa dunia hii waliopofushwa fikra zao na mungu wa dunia hii. Na ndiyo maana siku hizi movie zenye visa vya kindoa na kimapenzi zimekuwa nyingi sana huku zikiwa zimechanganywa na misingi feki ya kishetani ili kukupoteza wewe unayejifunza maisha ya ndoa kupitia movie hizo na magazeti hayo.
Wewe mtu wa Mungu ni lazima ujue kuwa ndoa imeanzishwa na Mungu mwenyewe, na baada ya kuanzisha alitoa mwongozo wa ndoa, kwahiyo wewe ni lazima uusome mwongozo huo.,
Unaweza kuniuliza, HUO MWONGOZO UKO WAPI?
Jibu rahisi tu 👉👉👉NDANI YA BIBLIA TU.
Unaweza kusoma vitabu vingi Lakini kitabu kamili chenye maana sahihi na kubwa ni BIBLIA.
Mungu akubariki Sana
Min. Mathayo Sudai
0744474230 /0628187291
Maoni
Chapisha Maoni