UJUE UTII

     SOMO KUHUSU UTII

Utii ni nini kibiblia?

Utii ni kitendo cha kukubali kufanya maelekezo au maagizo unayopewa na aliye na mamlaka ya juu Zaidi yako wewe bila kujali  linakubaliana na maamuzi yako au la!.

Lakini pamoja na hayo watu wengi hawajui kuwa utii unaweza pia kutanguliwa na isihesabiwe kuwa ni dhambi ya kutokutii mbele za Mungu, Lakini hiyo ni katika mazingira maalumu ambayo tutajifunza mbele kidogo katika somo letu hili.

Ili kujua ni wakati gani tunapaswa tusitii Ni vizuri kwanza tukawajua watu ambao biblia imetuagiza tuwatii wakati wote:

1 Utii kwa wazazi wetu:

Wakolosai 3:20  “Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana”

Hili ni agizo la Mungu kwa kila mwenye baba, au mama au mlezi, Mungu ametuagiza tuwatii wazazi wetu, kwa kila wanachotuelekeza kufanya. Na zipo baraka nyingi  katika kufanya hivyo  ikiwemo kupewa upendeleo wa kuishi umri mrefu hapa duniani

Kutoka 20:12 Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.

Hata Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa na utii huu ukisoma Luka 2:51 inasema .. “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.

Vivyo hivyo na sisi tunapaswa tuwe na huu utii kwa faida zetu wenyewe. Na pia kuyatimiza maagizo ya Mungu.


2 Utii kwa Mume:

Wake wamepewa maagizo ya kuwatii waume zao kwa kila namna.

1Petro 3:1 ” Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; ……5  Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. 6  Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote”

Soma pia Wakolosai 3:18 utaliona jambo hilo hilo.. Ikiwa wewe ni mke, halafu huisikii sauti ya mume wako labda kwasababu anakipato cha chini au anamapungufu fulani, au ni mwenye dhambi usidhani kuwa Mungu yupo upande wako. Unapaswa umtii na ujishushe kwasababu hayo ndiyo maagizo ya Mungu.


#3 Utii kwa wazee:

1Petro 5:5  “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu,..”

Mungu ametupa maagizo kama vijana, kuwathamini wazee, katika kanisa na vilevile katika jamii. Wanapotoa Mashauri hatupaswi kuwapinga au kujibishana nao,..Tukifanya hivyo tusidhani kuwa Mungu yupo upande wetu. Tunapaswa tuwape heshima kama vile wazazi wetu wenyewe ndivyo Mungu atakavyotufanikisha.


1Timotheo 5:17  Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha

1Timotheo 5.1  Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu;


#4 Utii kwa viongozi wetu wa Imani:

Bwana anatuagiza, tuwatii wale wanaotungoza katika njia ya wokovu. Na ndio maana Paulo alimwandikia Filemoni maneno haya:

Filemoni 1:21  “Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo”

Lakini tukipashana nao kauli au kuwavunjia heshima, au kutowasikiliza, basi tujue kuwa tunampinga Mungu, na Hivyo Mungu hawezi kuwa upande wetu hata katika huduma zetu.


#5 Utii kwa mabwana zetu (ma-boss):

Waefeso 6:5  “Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo;

6  wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;

7  kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;

8  mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru.”

Ikiwa utamvunjia heshima boss wako, ukafukuzwa kazi, usidhani kuwa Mungu atakuwa na wewe hata katika hiyo kazi nyingine mpya utakayokwenda kuitafuta. Haijalishi wewe ni mkristo au la..Maadamu umewekwa chini ya boss wako, basi huna budi kutii yale yote anayokuagiza kufanya bila unafiki..


#6 Utii kwa wenye mamlaka (Serikali):

Tito 3:1  “Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; 

2  wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.

Serikali na mamlaka zote zinafanya kazi ya Mungu, hivyo pale inapotuagiza tulipe kodi tunapaswa kufanya hivyo, inavyotuagiza tusifanye hiki au kile tunapaswa tutii..Lakini kama tutakwenda kinyume na serikali, kwa kiburi chetu wenyewe basi tujue kuwa Mungu hapo nasi hawezi kuwa na sisi.


#7 Utii kwa Mungu:

Huu ndio utii ulio wa juu Zaidi kuliko wote.. Biblia inatuambia katika Yakobo 4:7  “Basi mtiini Mungu…”.. Utii huu tunaweza kuuona  ukijidhihirishwa katika ukamilifu wote kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Wafilipi 2:7  “bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

 8  tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa MTII hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 

9  Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 

10  ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; 

11  na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

Inatuambia tena…

Waebrania 5:7  Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;

8  na, INGAWA NI MWANA, ALIJIFUNZA KUTII kwa mateso hayo yaliyompata;

9  naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;

Vivyo hivyo na sisi kila mmoja Maisha yetu yanapaswa yawe ya utii, tukilitii Neno la Mungu, kila tunapoagizwa tulifanye.

Swali

Lakini sasa Je! ninapaswa kuwatii wote hawa hata kama mmojawao anachoniambia kinakinzana na maagizo ya Mungu?

Jibu

Biblia imeweka wazi kabisa katika hali kama hiyo tunapaswa tusitii maagizo ya mtu yeyote bali ya Mungu kwanza..Ukisoma katika biblia utaona kuna wakati mitume walizuiliwa kuhubiri injili na wenye mamlaka na viongozi wa Dini lakini mitume walewale waliosema watiini wenye mamlaka ndio wakawa wa kwanza kusema..Imetupasa kumtii Mungu kuliko mwanadamu,


Matendo 5:27  “Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,

28  akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.

29  Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”

Leo hii mama au baba yako anaweza kukwambia ufanye mila za matambiko, Na huku wewe unajua kabisa jambo hilo linakinzana na maandiko, hapo hupaswi kumtii mzazi wako hata kama itaonekana amewavunjia heshima kiasi gani…


Wazazi

Au wazazi wanakushurutisha unywe pombe, au ufanye dhambi, hapo unaruhusiwa kutowatii kwasababu utii huo hautokani na Mungu na hivyo mbele za Mungu hutahesabika kuwa hajawatii wazazi wako.. Maandiko yanathibitisha hilo (Mathayo 10:37)

Serikali

Vilevile, Serikali imekupiga marufuku usiabudu. Au usihubiri injili, Hapo unapaswa usiitii serikali hata kama ni Mungu ndiye aliyeruhusu tutii mamlaka hizo. Ilimtokea Danieli, lakini yeye alihesabu mamlaka na Mungu ni kubwa kuliko mamlaka zote, hivyo alichofanya ni kufungua madirisha kabisa watu wote wamwone akiabudu, bila woga wowote, Na sisi vivyo hivyo hatupaswai kuogopa kuyashika maagizo ya Mungu Zaidi ya wanadamu.

Mume.

Au Mume, anakushurutisha mfanye tendo la ndoa kinyume cha maumbile, hapo hupaswi kumtii, mume wako, kwasababu maagizo hayo yanakinzana na Neno la Mungu, au aakushurutisha kufanya mambo kinyume na mapenzi ya Mungu, hapo hupaswi kutii. jambo la muhimu hapo ni kuishi na mume kwa hekima ya kimungu na umuombee, ili aponywe kwa neema uliyonayo wewe, usijaribu kufanya jambo la kumtii mwanadamu ukampuuzia Mungu. utiifu wa Mungu ni Zaidi ya utiifu mwingine wowote.

Au boss wako anakulazimisha uingie katika mikataba ya rushwa, Na huku unajijua kabisa kuwa unachofanya kinakinzana na Imani yako, hapo hupaswi kumkubalia, au anakulazimisha ufanya naye uzinzi, hapo pia hupaswi kumkubalia haijalishi ni boss wako anayeheshimika kiasi gani. Au maandiko yamekuagiza uwatii hao kiasi gani.

Hivyo UTIIFU wowote ni lazima upatane na maagizo ya Mungu, kama haukinzani na Neno la Mungu hapo unapaswa utii yote unayoelekezwa kwa moyo wote bila kiburi..Na ndivyo Mungu atakavyokufanikisha..

Kwasababu kinyume na hapo, ukosefu wa utiifu wowote, ni kazi ya shetani ambayo siku hizi za mwisho ndio umekita mizizi..

2 Timotheo 3:1  Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.2  Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, WASIOTII WAZAZI WAO, wasio na shukrani, wasio safi.


Je! Umeokoka?

Je ndani yako kiburi kimekaa? Je unajua kuwa watu wa namna hiyo hawataurithi uzima wa milele? Je Unafahamu kuwa tunaishi katika kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia, na hatutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili, Na unyakuo ni wakati wowote kwasababu dalili zote zimeshatimia?.. Kwanini usimpe leo Kristo NAFASI kuu kwenye Maisha yako.? Kwanini usiwe na uhakika wa kwenda mbinguni hata ukifa leo?

Kama upo tayari kufanya hivyo sasahivi.. basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, .

NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu, unatii sasa kwa kunayaacha na kujitenga nayo, Na Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la Mungu ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI