NITAMFANYIA MSAIDIZI…..
NITAMFANYIA MSAIDIZI..
Bwana Yesu asifiwe watoto wa MUNGU. Leo naomba tujifunze jambo moja fupi sana lenye msingi sana kwa mabinti na vijana ambao wapo katika mchakato wa kupata wenza wao wa maisha yaani kuifikia ndoa. Imekuwa kama desturi ya kila mtu mwenye uhitaji wa kuoa au kuolewa, kuwa na shauku tu ya kuangalia sifa zile anazozihitaji yeye, bila hata kujali sifa za msingi za awali ambazo kwa kuzishika hizo, mwanadamu anao uwezo wa kupata mwenza kamili kwa ajili ya maisha yake.
Biblia inasema
Mwanzo 2:18 “BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu akae peke yake, NITAMFANYIA MSAIDIZI wa kufanana naye”
Hapo ukipasoma vizuri utagundua kuwa Mungu kazungumza mambo machache ya muhimu sana ambayo ukiyajua yatakushindia. Karibu tuyaone.
1. SI VEMA MTU AKAE PEKE YAKE
Sasa jambo la msingi hapa ni kwamba, Mungu mwenyewe anatambua kwamba, haipendezi mwanadamu akae peke yake. Maana yake suala la mtu kuwa na mwenza, ni jambo jema sana mbele ya macho ya Mungu. Hapa Mungu aliona ndege wa angani, na wanyama wengine si wa thamani sana kama alivyo mwanadamu. Sasa kama wanyama aliwaumba wawili wawili, iwenye mwanadamu awe peke yake.? Na ndiyo maana hata katika waebrania alisema.. Ndoa na iheshimiwe na kila mtu… kwa sababu inalenga kumfanya mtu mmoja kuwa na mwenza na kuinyanyua thamani ya mwanadamu huyu ambaye hapo mwanzo alikuwa mwenyewe.
Kwa hiyo hata mtu kuchukua jukumu la kuifikiria ndoa hata kama hana mpango wowote basi atambue kuwa analifikiria jambo jema sana machoni pa mtu.
Na kukaa peke yako, ni jambo ambalo si salama sana kwa maisha yako kama mkristo, maana linaweza kukufanya kupotelea kabisa kwenye moto wa jehanamu dhambi ya kuwaka tamaa
1 Wakorintho 7: 8 “ Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni AFADHALI KUOA KULIKO KUWAKA TAMAA. Unaona Paulo anazungumzia kuhusu tamaa kwamba kwa kukaa bila kuoa au kuolewa kuna hatari kubwa sana ya kuanza kumtamani kijana kwa ngono au kumtamani msichana, pale tu utakaposhindwa kustahimili. Na ndiyo maana Yesu alisema uzinzi si mpaka ulale na mtu, hata kwa kumtamani tu kwa tamaa ya ngono unakuwa tayari umesha zini naye.
Na hili tunaliona hata leo kwa vijana wengi, wakikaa unakuta wanasimuliana habari za ngono tu jambo linalofanya tamaa kuwaka. Lakini Biblia inasema heri kuoa kuliko kufanya hayo. Maana wazinzi wote sehemu yao ni katika ziwa la moto, ufunuo 21:8.
2. NITAMFANYIA MSAIDIZI
Jambo la pili ambalo ni ahadi ya Mungu kwa kijana wa kiume aliye peke yake ni kwamba, NITAMFANYIA MSAIDIZI.
Jambo hili ni la msingi sana kwa vijana na mabinti kulifahamu maana limebeba jicho na msingi kwa yule unaye muhitaji. Kwa vijana wa kiume ni lazima atambue kuwa mke ni msaidizi wake.
Hebu jiulize kidogo, nini maana ya msaidizi.
· Ni mtu ambaye anakusaidia majukumu yako
· Ni mtu ambaye anazifanya kazi zako usipokuwepo
· Ni mtu ambaye anaweza kufanya kazi yako pale unapokuwa unafanya nyingine
· Ni mtu ambaye kama ni kazini, basi ana cheo kidogo kuliko wewe
· Ni mtu ambaye anapokea maelekezo kutoka kwako
· Ni mtu ambaye anatakiwa kukutarifu jambo la kiofisi alilolifanya au analotaraji kulifanya,
· Ni mtu ambaye analinda nafasi na heshima ya boss wake. n.k..
Sasa kijana kabla hajaoa, basi lazima atambue kuwa anamtafuta mtu ambaye atasimama katika nafasi hizo zote na kwa mantiki hiyo ni lazima kijana huyo awe katika mazingira za kuzibeba sifa hizo zote za msaidizi huyo.
Lakini Biblia inamtaja mwanamke kuwa ndiye msaidizi kwa mwanaume. Hiyo imsaidie binti kutambua jukumu lake anapomuhitaji mume na ya kwamba anapaswa kusimama katika nafasi hizo. Naye kijana ni lazima ajue kuwa anatakiwa kuishi na mwenza wake katika ustadi na ufundi ili kuweza kumlinda na kumtunza katika sifa zake zote alizonazo kama msaidizi. Na ndiyo maana Biblia inasema..
1 Petro 3:7 “Na ninyi waume, KAENI NA WAKE ZENU KWA AKILI; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”.
Hapo amesema KAENI NA WAKE ZENU KWA AKILI akiwa na maana kuwa uishi kwa kutambua sifa za mke/msaidizi ili isije ikakugharimu. Na anasema KAMA CHOMBO KISICHO NA NGUVU, akiwa na maana kuwa katika kuishi na mke yeye ni Msaidizi wako. Si Mwenye nguvu Kama mume
Lakini kuna hatari kubwa sana pale kijana atakaposhindwa kuishi kwa kutambua nafasi ya msaidizi wake. Na Biblia imesema hatari hiyo ni kuzuiliwa kwa maombi ya mume anapoomba, kwasababu atakaposhindwa kuishi naye kwa akili basi ataruhusu matatizo na makwazo katika ndoa na hata kufukuza sikio la Mungu kwake. ISAYA 59:1.
Mke ni LANGO katika familia, asipokaa sawa basi anaweza kuzuia kila aina ya maendeleo katika familia. Kuwa makini sana kijana.
Sasa hii ikusaidie kijana kutambua kuwa mke ni msaidizi wako na pia unapaswa kuwa na maarifa mengi kuliko yeye, nguvu ya hekima kuliko yeye, akili kuliko yeye, ubunifu kuliko yeye, nguvu ya maombi kuliko yeye, ufahamu wa kimungu kuliko yeye, ili yeye awe msaidizi kamili kwako, na kwamba awe msaidiaji wa yale uliyonayo wewe. Na ndiyo maana Biblia ikasema mume ni kichwa cha familia.
Pale kijana atakapokuwa amemuoa mke aliyemzidi kila kitu basi atambue kuna hatari kubwa sana katika ndoa hiyo maana, msaidizi ndiye atakayekuwa mtenda kazi mkuu na yeye sijui atakuwa katika nafasi gani. Namuomba Mungu akuponye wewe kijana.
Kuna maajabu yapo kwenye familia zetu, utakuta hata habari za maombi, mke ndiye anamsisitiza baba, mke ndiye anamfundisha baba neno la Mungu halafu mume yupo tu anaongozwa, si mbaya sana kwa ufalme wa Mungu lakini ni jambo la aibu sana mke kuwa kiongozi wa familia.
Hebu tusome hapa ….1 Wakorintho 14:35 “Nao wakitaka kujifunza neno lolote , na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa”
Hebu tafakari Paulo alivyowaambia wanawake wa korintho wajifunze kwa waume zao, majumbani, lakini kumbe nyumbani kwenyewe mwanaume naye unakuta hajui kitu, unafikiri nini kinafuata. Kwahiyo mwanaume lazima awe na maarifa zaidi kuliko mke, na ndiyo maana hata kabla ya mwanamke kuumbwa Mungu alikuwa ameshampa Adamu maarifa na majukumu. Hata Eva alipokuja alikuta mumewe amejaa maarifa ya Mungu naye akaanza kujifunza kwake.
Lakini pia kwa binti unayehitaji kuolewa basi ni lazima uwe na jicho la kutambua kuwa wewe utasimama katika nafasi ya msaidizi na si mtenda kazi mkuu. Utasimama kuyabeba maono ya mume wako, kumshauri kwa yale aliyonayo na hata kumsaidia mume katika kubuni na kutafuta mbinu sahihi za mafanikio
Mke ni mtu ambaye anapaswa kuwa mwana maombi mzuri maana yeye ni lango la familia.
Jambo la msingi ambalo ni tatizo katika ndoa nyingi za leo ni kwamba, katika familia wanaume wengi, wanasimama nafasi za wake zao na wanawake wanasimama nafasi ya baba, ni hatari kubwa sana hii.
Binti wa Kristo uliyeokoka, kabla hujachukua uamuzi wa kuingia kwenye ndoa na kijana basi tambua wewe ni nani katika ndoa, na pia hakikisha unauhakika ya kwamba huyo mwenza wako ataweza kusimama katika nafasi yake. Ogopa kusimama kwenye nafasi ya mumeo utakufa. WEWE NI MSAIDIZI WAKE.
3. WA KUFANANA NAYE
Hiki ni kipengele cha mwisho katika ujumbe huu, WA KUFANANA NAYE.
Kumbe Mungu kabla hajamleta Eva kwa Adamu, alikuwa amesema atamleta msaidizi anayefanana na Adamu. Tafakari vizuri hapa, ni kwamba… SI MTU TU, KISA MTU; bali ni yule wa kufanana naye. Kwa hiyo kijana na binti ambaye bado hujaingia kwenye ndoa, ni lazima uwe na jicho la kumjua mtu mnayeendana naye.
Kama ni kijana pata binti ambaye ukiwa naye ataweza kusimama katika sifa zile zote za msimamizi na kwamba ulivyo wewe na yeye mnaendana yaani unafanana naye maana ndiye Mungu aliyesema hivyo kwamba msaidizi wa kufanana naye. Sasa kumbe kama ,msaidizi anafanana na Bosi, basi kumbe na Bosi naye lazima afanane na msaidizi.
Kama ni kijana usimuangalie tu binti wa watu, eti kwasababu ni mcha Mungu sana, basi ukaona anakufaa, noo, lazima utafakari je wewe una sifa za kuwa na msaidizi kama yeye?. Leo hii vijana wengi wahuni wa mtaani, ambao hawawezi kuwa na mke mmoja, hawaridhiki mpaka waonje na nje, eti wanapenda wanawake wenye heshima na nidhamu na waliotulia, sasa unaweza ukakaa ukajiuliza kuwa kwanini anapenda binti aliyetulia angali yeye hajatulia?, mwisho wa siku jambo hili linawafanya mabinti ambao walikuwa na maadili yao mazuri, kuanza kuteseka na hata kuona ndoa chungu, mwishi wa siku kuacha wokovu. Haya yote ni kwasababu kijana huyu alimtafuta mtu ambaye hafanani naye.
Pia binti lazima ujue je huyu anayetaka kunioa, anafanana na mimi? Na hii ndiyo sababu Mungu alikataza wana wa israeli wasiwaoe watu wa mataifa mengine. Tambua kwamba ukikubali kujipachika sehemu ambayo si yako basi utaambulia kupigwa na kulia kila siku kwasababu umekubali kuolewa na mtu USIYEFANANA NAYE.
Ni maombi yangu kuwa haya mambo matatu yaliyonenwa na Mungu mwenyewe, utayaelewa na kuyafanyia kazi wewe binti na kijana wa kristo.
Mimi ni Minister Mathayo Daudi Sudai niliye mdogo kuliko wote.
Na Mungu akubariki.
0744474230/ 0628187291
Youtube: Minister Mathayo Sudai
Aminaa Mungu akubariki kwa somo zuri mtumishi
JibuFuta