JE NI KWELI THAWABU YAKO IPO?

 


              
   JE NI KWELI THAWABU YAKO IPO?

Bwana Yesu asifiwe watu wa MUNGU.

Leo naomba tujikumbushe jambo moja la msingi sana, ambalo ndilo tumaini la kila mmoja katika maisha yake ya kuabudu au kumtafuta Mungu. Wengi husema wapo katika safari ya kuelekea mbinguni, baada ya kazi ya hapa duniani kwisha.

Biblia inatuambia kwamba watakaoshinda maisha ya hapa duniani, watapata thawabu, ambayo ni kama malipo makubwa sana ya maisha yao ya utakatifu hapa duniani.

       Mathayo 5:12 “Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; …

Siku zote watu wanaabudu na kufanya ibada zao kwa lengo hili la kukaa pamoja na Bwana katika nyakati zinazokuja, huku wakiamini kuwa watapata thawabu.

Lakini kwako wewe, JE NI KWELI THAWABU YAKO IPO?

   Hebu tujifunze jambo kupitia mstari huu wa Biblia

     Mithali 28:9 “ Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo”

Unaona hapo Biblia inatuambia kuwa mtu yeyote asiyeweza kuelekeza sikio lake kuisikia amri ya Mungu na kuyaishi yale yaliyoagizwa na Mungu, basi atambue kuwa hata maombi  na ibada yake anayofanya ni chukizo mbele za Mungu. Mtu ambaye ataacha kuishika amri ya Mungu, na akaendelea kumuomba Mungu, kufanya ibada basi atambue kuwa anafanya machukizo mbele za Mungu wetu, na ndiyo maana Paulo akamwambia Timotheo kwamba, Maana utakuja wakati, watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu wao makundi makundi kwa kuwa wana masikio ya utafiti. 2 Timotheo 4:3.

Kwahiyo kumbe kunawakati watu wanageuza kabisa masikio yao, na kuanza kusikia mafundisho tofauti na mafundisho ya Mungu. Na ndiyo maana hata leo utaona kuna watu ambao wanakimbilia kwenye miujiza tu na ishara zinazoonekana kwa watu wanaoitwa manabii wa leo, lakini hawataki kusikiliza mafundisho yanayowaonya, yanayowafundisha na kuwakemea, huko nikujitenga na imani na kuyakataa mafundisho ya uzima kama vile Paulo alivyotabiri kwa Timotheo.

Lakini kumbuka Mithali 28:9 kwamba yeye ageuzaye sikio lake asiisikie sheria , hata maombi yake tu ni chukizo mbele za Mungu.

Hebu tazama maneno haya ya mwandishi wa zaburi katika

 Zaburi 66:17-18 “ Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu. Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia”.

Daudi anatuambia hata kwa kuwaza mabaya tu, kunatufanya maombi yetu yasisikike. Sasa tafakari kwa habari ya dunia ya leo, tazama jinsi watu wengi wanavyoingia makanisani kwa desturi yao lakini baadae watu haohao unawakuta kwenye disko, hao hao unawakuta wanalewa, wasengenyaji, wachoyo, watu watukanaji, wezi, wazinzi, wao ndiyo waangaliaji wazuri wa picha za uchi, nyimbo za kidunia zimejaa kwenye simu zao, lakini hao hao unakuta wanajiita watumishi, ukikutana nao salamu yao ni Bwana Asifiwe.   Sasa watu kama hawa mioyo yao na masikio yao yameacha kuisikia na kuishika amri ya Mungu lakini wameshikamana na mambo ya dunia, huku wakisema wapo katika safari ya kuelekea mbinguni; wanaangamia kwa kukosa maarifa.

Mimi siku zote huwa nasema kuwa wapo watu wengi ambao wanaamini kuna taji zimeandaliwa kwa ajili yao huko mbinguni lakini kimsingi watashangazwa sana na kile watakachokipata, maana kitakuwa ni tofauti na kile wanachokiamini leo, kwasababu wamemshika Kristo kwa maneno yao lakini mioyo yao ipo duniani, nao wamegeuza masikio yao na kufanya machukizo mbele za Mungu. Na ndiyo maana Yesu akawaita wanafiki.

     Mathayo 15: 7-9 “ Enyi Wanafiki, ni vema alivyotabiri  Isaya kwa habari zenu, akisema, WATU HAWA HUNIHESHIMU KWA MIDOMO; ILA MIOYO YAO IKO MBALI NAMI. NAO WANIABUDU BURE, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu”.

 Sasa ni lazima watu tujichunguze nafsini mwetu kwamba je kile tunachokitazamia ndivyo tutakavyo kipokea?. Maana waweza kuwa unaishi kama mkristo ukiamini kuwa utapata thawabu mbinguni, kumbe unajidanganya mwenyewe. Yesu aliliona hili ya kwamba watu wanaweza kuishi kwa matarajio hayo kumbe wanajidanganya wenyewe, kwa kuwa wanashindwa kuitii sheria ya Mungu mioyoni mwao, ila wanaabudu kwa midomo tu.

Luka 13:25-27 Biblia inasema “wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama na kuubisha mlango, mkisema Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulitufundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

Hebu tafakari maneno hayo, Wakati watu wanajiona wakristo kwa kuwa wanahudhulia kanisani, kumbe Kristo anawaona kuwa ni watu wafanyaji wa udhalimu.

Hii yote ni kwasababu wamegeuza masikio wasiisikie amri ya Mungu, hawataki kufanya mapenzi ya Mungu, ni wakristo vuguvugu. Kwahiyo kile wanachokitazamia ni tofauti na hiki wanachokifanya leo.  Ni upotezaji wa Muda ni heri wangeacha.

Na wewe msomaji wangu naomba chukua wakati wa kujiuliza kuwa JE! THAWABU YAKO IPO KWELI? Isije kuwa unapoteza muda kama hawa ambao Yesu atawakataa kwa udhalimu wao. Itakuwa ni hasara kubwa kufikiri kuwa unaingia mbinguni, kumbe unaingia jehanamu. Jambo la msingi ni kugeuza sikio lako liisikie sheria ya Mungu na moyo wako uihifadhi amri ya Mungu. Usjiaribu kuishi kwa kuambatana na mambo ya dunia hii, utapotea.

   Kama unaona ndani ya moyo wako kuna udhalimu na umeshikamana na dunia basi tambua dua na sala zako ni chukizo, yaani Mungu hazisikii, kwasababu Mungu hapendezwi na mtu anayetumika kwa mabwana wawili, Mungu na Ibilisi.

JE UPO SALAMA? Kama la!,,,je! unahitaji kuwa salama?, basi chukua nafasi tafakari, tafuta mahali penye utulivu kisha mwambie Mungu sala hii kwa imani.

BABA YANGU, MUNGU UISHIYE MILELE,WEWE NI BWANA ULIYEUMBA VYOTE VINAVYOONEKANA NA VISIVYOONEKANA, WEWE NI MKUU NA HAKUNA MWINGINE KAMA WEWE. NINAJUA YA KUWA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI NA UDHALIMU MWINGI UPO NDANI YA MOYO WANGU; LAKINI UMESEMA UNAWAREHEMU MAELFU NA MAELFU WANAOKUJA KWAKO, NAMI NINAOMBA NIREHEMU NA UNIOSHE KWA DAMU YA YESU, KWA AKIILI YANGU YOTE NINAKIRI YAKWAMBA WEWE NDIYE UNITAKASAYE KWA DAMU YAKO, HAKUNA MWINGINE. NAMI NINAOMBA TOBA KWAAJIRI YA YOTE NILIYOYATENDA KINYUME NA SHERIA YAKO. NINAOMBA KUSIMAMA UPYA KWA NGUVU ZAKO MUNGU WANGU ULIYE JUU. NINAAMINI KWAMBA KWA DAMU YAKO UMENIOSHA NA KUNISAMEHE UOVU WANGU WOTE, NAMI NAOMBA UNISAIDIE. NINAKUSHUKURU KWA UPENDO WAKO WA AJABU MUNGU WANGU UNIPENDAYE, NINAOMBA NA KUAMINI KUPITIA JINA LAKO YESU, AMINA.

Kama umefanya sala hii kwa imani na kumaanisha kuacha dhambi, basi anza kuishi kwa kuitii amri ya Mungu na ishi sawasawa na mapenzi yake. Achana na mambo ya dunia hii ambayo ni udhalimu mtupu na mgeukie Kristo, hapo utaanza kuitengeneza thawabu yako ya milele huko mbinguni.

 

   Mimi ni Mathayo Sudai niliye mdogo kuliko wote, na Mungu akubariki.

       0744474230/0628187291

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI