TABIA HATARISHI KWA MWANAMKE KATIKA MAHUSIANO,UCHUMBA HADI NDOA


 TABIA HATARISHI KWA MWANAMKE KATIKA MAHUSIANO,UCHUMBA HADI NDOA

Ungana na mimi Mathayo Sudai.

KWELI KUU: Tabia ni msingi na kielelezo cha mahusiano bora ya aina yoyote na hasa yale ya uchumba hadi ndoa.

Mithali 31:30:

Upendeleo hudanganya, na uzuri (wa sura au umbo au rangi) ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.​

Somo hili ni kwa ajili ya wanaume lakini pia ni kwa ajili ya wanawake. Kwa wanaume linawasaidia kujua mwanamke wa tabia gani ni wa kuoa na wa tabia gani si wa kuoa. Kwa wanawake linawasaidia kujichunguza na kubadilika kitabia ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa na mahusiano bora kuanzia hatua ya urafiki, uchumba hadi ndoa.

Tabia ni utambulisho wa kwanza wa mtu, ndio iliyobeba sura ya ndani ya mtu husika. Pamoja na kuwa mtu ana sura na umbo la nje linalomtofautisha na wengine na kumtambulisha lakini pia ni muhimu sote tukaelewa kuwa mtu si yule wa nje bali ni yule wa ndani ambaye wakati wote hutambulishwa na atabia yake aliyonayo, kuwa ni mtu mwema au mwovu, ni mzuri au ni mbaya, anafaa au hafai, anastahili au hastahili. Tabia ni utambulisho unaompa mtu nafasi ya kuishi vizuri na watu miongoni mwa watu kila mahali anapokuwepo.

Watu hawahitaji sura nzuri au umbo zuri kuishi na mtu, bali wanahitaji tabia njema ya mtu kuishi naye mtu huyo. Ni tabia yako ndiyo inakuwezesha kuwa na mahusiano mazuri na watu, tabia yako njema inakupatanisha na watu wanaokuzunguka na kukufanya uishi nao vizuri bila matatizo yoyote na hata yakiwepo ni rahisi kutatuliwa kwa sababu ya tabia yako njema.

Katika somo letu la leo nataka tuangalie kuhusu “Tabia hatarishi (kwa mwanamke) na hata kwa mwanaume katika mahusiano” ambazo zinaweza kuwa kizuizi hasa kwa mwanamke kuolewa iwapo atakuwa nazo na mwanamke ambaye amekwisha kuolewa kushindwa kuishi na mumewe. Leo nitazungumza na wanawake zaidi, na siku nyingine nitakapopata nafasi nitazungumza na wanaume pia.

Tabia namba moja: KELELE au MANENO MENGI:

Tabia hii ni matokeo ya upumbavu ambao unakuwa ndani ya mwanamke. Siku zote mwanamke mpumbavu hupiga kelele au huwa na maneno mengi yasiyo na maana katika maisha yake isipokuwa ni maneno ya umbea tu na usengenyaji, uchochezi na uchongezi pamoja na uzushi. Kabla hatujaendelea hebu tuyachunguze maandiko yafuatayo;

Mithali 9:13 – 16

[13] Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu,

[14] Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,

[15] Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao.​

Katika maandiko haya hapo juu sifa za mwanamke mpumbavu zimetajwa, na sifa hizi ni tabia anazokuwanazo mwanamke mpumbavu. Tutaangalia moja baada ya nyingine japo kwa kifupi sana ili kupanua ufahamu wetu.

Sifa ya Kwanza: Hupiga kelele:

Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, hana utulivu hata kidogo, wakati wote sauti yake imejaa ukali, hupayuka hata kama wewe unaongea kwa sauti ya chini, hana usiri katika mazungumzo yake, hutoa sauti yake kwa nguvu, hupaza sauti yake kwa nguvu, hutaka kila mtu asikie mnachozungumza na hasa kile asemacho yeye. Mwanamke wa namna hii hata kama utazungumza naye mkiwa chumbani lazima tu maneno yale yatasikika mpaka mtaa wa pili; kwa kadiri utakavyokuwa ukimnyamazisha ndivyo atakavyokuwa akizidi kupiga kelele.

Wanawake wamejaliwa sana kuongea, wana uwezo wa kuzungumza, ni wanawake tu wenye hekima ndio hutumia uwezo huu vizuri, lakini kwa wapumbavu kila anapofungua kinywa chake maneno yake ni kelele masikioni mwa wanaosikia, hayana msaada isipokuwa uharibifu. Ni hatari sana kuoa mwanamke wa namna hii. Mwanamke anayependa umbea, usengenyaji, uzushi, lawama, malalamiko, manung’uniko, matukano na kelele asiyekuwa na staha, utulivu, ustahimilivu, na hali ya kujizuia.

Hata hivyo uzoefu unaonyesha kwamba, ndoa nyingi zina migogoro isiyoisha na nyingine zinavunjika ikiwa ni pamoja na wanawake kupigwa na waume zao kwa sababu ya midomo yao (kelele zao) wanapoongea na waume zao. Hii ndio sababu Biblia inasema kuwa, Mwanamke mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe. Mwanamke usipokuwa na hekima utatumia kinywa chako kujiharibia mwenyewe.

Mwanaume mwenye akili njema hawezi kuoa mwanamke anayepiga kelele tu, hajui kuongea kwa hekima na kutenda kwa hekima. Mpumbavu hana kazi ila ana maneno mengi na uvivu umo ndani yake, ni sawa kabisa na mwanamke mpumbavu, hajui kufanya kazi njema ila anajua kuongea sana, kulalamika, kushutumu, kunung’unika, kutukana, kutusi, na kadhalika.

Wewe kama mwanamke una makelele napenda kukupa taarifa mapema kwamba itakuwa kwako vigumu kuolewa na mume bora na kama umeolewa siku za ndoa yako zinahesabika na pengine tayari hakuna utulivu wala amani ndani ya ndoa yako.

Biblia inasema kuwa, Jawabu la upole hugeuza hasira, bali neno liumizalo huchochea ghadhabu (Mithali 15:1). Jawabu la upole ni zao la hekima, mpumbavu siku zote ana neno liumizalo (kelele) kinywani mwake na kwa sababu hiyo huchochea ghadhabu.

Pia Biblia inasema, Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; na mwenye roho ya utulivu ana busara (Mithali 17:27) Mpiga kelele hana uwezo wa kuzuia maneno yake, lakini pia hana roho ya utulivu ndani yake, kila atakalolisikia lazima alipigie kelele tena mahali palipo na watu wengi na atahakikisha kuwa kila mmoja amesikia. Mwanamke wa hivi yuko hatarini kutokuolewa na kama ameolewa basi ndoa yake haitakaa iwe na amani.

Sifa ya Pili: Ni mjinga, hajui kitu:

Mwanamke mpumbavu ni mjinga, hajui kitu. Mjinga ni mtu aliyekosa maarifa, ni mtu asiyejua kitu, hajui nini ni nini na lipi limpasalo kutenda kwa wakati gani ili kujenga na wala si kubomoa. Mwanamke mjinga asiyejua kitu hajui kuwajibu watu vizuri, ajui kuweka na kutunza siri, hajui kuwastahi watu, hajui kuitawala hasira yake, hajui kujizuia, hajui kuheshimu na kuwatii watu wengine, hajui kuwatanguliza wengine, yaani hajui kitu chochote chema, amechagua njia ya ujinga kwa kuwa mpumbavu.

Ni ngumu sana mwanamke asiyejua kitu chochote chema kuolewa au kudumu katika ndoa, na kama atadumu basi ndoa yake haitakuwa na amani daima labda abadilike. Mwanamke mwenye hekima anayo maarifa, anajua jema la kutenda na wakati wa kulitenda, mambo yake yapo kwenye mpangilio maalumu unaoleta maana katika maisha yake na maisha ya wengine wote wanaomzunguka. Mwanamke mjinga ni shida kwa wengine, lakini mwenye maarifa ni baraka kwa wengine, kila mmoja umfurahia na hupenda kuwa karibu naye, lakini mpumbavu kila anapokuwa karibu na watu husababisha tatizo.

Usiwe mwanamke mjinga asiyejua kitu. Watu wasiojua kitu maneno yao huwa ni kelele masikioni mwa watu kwa sababu hayawasaidii ila kusababisha matatizo tu kama sio kuwapotezea muda wao. Mwanamke asiyejua kitu si mtendaji ila ni mpiga kelele tu, ana maneno mengi lakini hana matendo kabisa na maneno yake wakati mwingi kama sio wote huelekea uharibifu kwa sababu hajui kitu. Mwanamke wa aina hii ni ngumu kuolewa na ni ngumu kudumu katika ndoa au kuwa na ndoa ya amani na utulivu.

Tabia namba mbili: HASIRA YA HARAKA:

Mithali 14:1

Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.

Unaweza kuona ni kitu cha kawaida sana wewe kuwa na hasira za haraka lakini ukweli ni kwamba si kitu cha kawaida kwa sababu kinapelekea wewe kutenda mambo kwa ujinga lakini pia inasababisha wewe kuogopwa na watu na watu hao wakuzire.

Kwa upande mwingine Biblia inasema, Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi, bali mwenye roho ya hamaki (yaani anayefanya haraka kukasirika) hutukuza upumbavu (Mithali 14:19). Asiyefanya haraka kukasirika ana fahamu nyingi kwa sababu atatenda kwa busara lakini mwenye kufanya haraka kukasirika huwa mjinga, hutukuza upumbavu kwa kutenda kwa upumbavu na mtu wa namna hii huzirwa na watu, watu humuogopa na humkibia kabisa.

Lakini pia ikumbukwe kuwa Biblia inasema kwamba, Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano (Mithali 15:18). Ulishamkuta mwanamke mwenye hasira akigombana? Hataki hata kuamliwa na mtu yeyote, kwa kadiri unavyoamua ugomvi ndivyo anavyozidi kuongeza hasira zake na kuchochea ugomvi.

Hakuna mtu anayependa ugomvi, kila mmoja anapenda amani, kwa hiyo mchochezi wa ugomvi hapendwi hata siku moja na huyo ni mtu aliye mwepesi wa hasira. Watu wakishajua kuwa wewe ni mgomvi hukuepuka ingali mapema sana. Ni ngumu sana mwanamke mwenye hasira kuolewa kwa sababu bila shaka atakuwa mgomvi, na hakuna mwanaume anayependa ugomvi (pia hakuna mwanamke anayependa ugomvi) isipokuwa mgomvi mwenyewe. Ni mgomvi tu tena mwenye hasira ndiye apendaye ugomvi.

Mwenye hasira au mwepesi wa hasira ni mgomvi. Siku zote mtu anayefanya haraka kukasirika huwa ni mgomvi, na huchochea ugomvi hata mahali ambapo hapakuwa na ulazima wa watu kugombana. Kwa kuwa ndani yake ana hasira za karibu ugomvi ni maisha yake kila akasirikapo, na mtu wa namna hii hawezi kuishi na watu kwa amani, lazima watu watamuepuka na kumkimbia kila wamwonapo.

Mithali 22:24, 25 anasema, Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi. Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia nafsi yako mtego. Wawili hawawezi kutembea njia moja wasipo patana.

Andiko hili maana yake ni kwamba, usiwe kwenye mahusiano na mtu mwenye hasira nyingi, wala usitembee au usiende katika hali hiyo ya mahusiano na mtu mwenye ghadhabu nyingi, kwa sababu ni lazima mahusiano yako na mtu huyo yatasababisha matatizo katika maisha yako. Au pengine atakukosesha na kukusababisha ufanye vitu ambavyo hukupaswa kufanya vilivyo kinyume. Au pengine atakuambukiza tabia zake zitokanazo na hasira yake nawe ukawa mwenye hasira kama yeye. Hasira huambukizwa iwapo tu utakuwa kwenye mahusiano na mtu mwenye hasira.


Mwanamke mwenye hasira anajiweka kwenye hatari ya kutokuolewa. Mwanaume yeyote mwenye akili hawezi kuoa mwanamke mwenye hasira hata siku moja kwa sababu anajua kuwa kuoa mwanamke huyo ni kwa hasara yake mwenyewe.

Tabia namba tatu: KUPENDA FEDHA:

1Timotheo 6:10

Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.​

Fedha haina ubaya wowote kwa sababu fedha ni jawabu la mambo yote katika hii dunia (Muhubiri 10:19), ubaya na tatizo lipo katika hali au tabia ya kupenda fedha. Ni mbaya sana mtu kupenda fedha, ni mbaya sana. Na hii ni tabia inayokuwa ikiambatana na mtu ndani ya moyo wake. Ikumbukwe kuwa upendo hutokea moyoni, na tabia mara zote hujengwa moyoni. Kwa hiyo kupenda fedha ni tabia inayoishi ndani ya mtu na humtambulisha mtu huyo kuwa ni wa namna gani.

Kabla sijaendelea mbele sana, napenda tuangalie mambo mawili makubwa yaliyotajwa katika msitari wetu hapo juu kuhusu fedha na mtu ambayo ni hatari sana na yote hutokea ndani.

Jambo la Kwanza: Upendo dhidi ya fedha (yaani kupenda fedha)

Ni muhimu tukaelewa kwamba, kuna upendo wa namna nzuri na pia kuna upendo wa namna mbaya, upendo wa fedha unaotajwa hapa ni ule wa namna mbaya ambao unavuka mipaka ya Neno, kusudi na mapenzi ya Mungu katika maisha yako na maisha ya wengine. Kwa vyovyote vile uwe ule wa namna nzuri unaobaki katika mipaka ya Neno, mapenzi na kusudi la Mungu au ule wa namna mbaya bado upendo una tabia moja katika utendaji wake ndani ya moyo au nafsi.

Upendo ni hatari sana kwa sababu hauwezi kutenganishwa na moyo wa mtu au nafsi ya mtu, umeshikamana na mtu ambaye anao. Hii ndio sababu upendo wowote haujawahi kumwacha mtu salama.

Katika kitabu cha Wimbo Ulio Bora 8:7, Biblia inasema, “Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha….” Hii ni tabia ya upendo wowote unapokuwa ni upendo wa kweli kabisa na si wa kinafiki, na ndio maana hata Mtume Paulo akiwaandikia Warumi anasema kuwa, Ni nani atakayetutenga na upendo wa Mungu Baba uliyo katika Kristo Yesu?, kisha anaendelea kwa kusema hakuna kitakachotutenga na upendo wa Mungu. Kwa nini? Kwa sababu upendo una nguvu kuliko vitu vyote.

Mungu kwa sababu ya upendo wake kwa ulimwengu alimtoa mwanawe pekee Yesu na hakuna kilichoweza kusimama kinyume chake ili kuzuia upendo huo. Yesu pia kwa jinsi alivyotupenda upeo alijitoa mwenyewe kufa msalabani kwa ajili yetu wenye dhambi, na hakuna kilichostahimili kusimama kinyume chake kuuzuia upendo huo. Upendo una nguvu hata nguvu ya maji haiwezi kuuzima, hata nguvu ya mito haiwezi kuuzamisha.

Sasa hebu fikiria juu ya mtu anayependa fedha, kwa sababu ya ule upendo wake katika fedha atakuwa tayari kulipa gharama yoyote ile kuipata fedha, na kwa sababu upendo hauzimishwi wala kuzamishwa, hakuna awezaye kumzuia.

Popote palipo na upendo wa kweli pana dhabihu, na hakuna awezaye kuzuia nguvu ya dhabihu, huo ndio uzuri na ubaya wa upendo, ni uzuri kama upendo huo utaangukia mahali sahihi, na ni ubaya iwapo upendo huo utaangukia mahali pasipo sahihi (pabaya na paovu). Kupenda fedha ni hatari sana tena sana kwa sababu ni shina la mabaya ya kila namna.

Jambo la Pili: Tamaa (Tamaa ya fedha)

Palipo na kupenda fedha tamaa ya fedha huwa haikosi. Hii huwa ni tamaa ya kumiliki (possess) fedha hasa ya mtu mwingine ambayo wewe hujaitolea jasho. Tamaa ya namna hii pia haijawahi kumuacha mtu salama kabisa, huzaa mabaya yanayopelekea kumuondoa mtu katika imani, ni tamaa inayoleta mafarakano ya mtu na imani yake kwa Mungu (wokovu).

Tamaa ya fedha na kupenda fedha ni kama roho na pumzi, huwezi kuvitenga kimoja kutoka kwa mwenzake. Kama una tabia ya kupenda fedha basi una tabia ya kutamani fedha, na hii ni shida inayoleta shida katika mahusiano.


TUREJEE KWA MWANAMKE:

Mwanamke huwa na tamaa ya kuwa na vitu vizuri, hata Hawa alipoona ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, alitamani baada ya kutazama sana. Tamaa ni nzuri inapokuwa inatawaliwa na Neno la Mungu, ni nzuri iwapo haivuki mipaka ya Neno la Mungu, lakini inapofikia mahali ikavuka mipaka ya Neno la Mungu tamaa mbaya huzaliwa mara. Na tamaa mbaya inapozaliwa, upendo usio sawa huzaliwa.


Kwa sababu fedha ni jawabu la mambo yote, na mwanamke hutamani vitu vizuri, anapokosa kiasi na kujitawala, atajikuta anapenda fedha kwa sababu akiwa na fedha atakuwa na kila kitu anachokitamani. Na roho ya kupenda fedha inapoingia ndani yake kwa sababu ya tamaa zake, huwa na shahuku ya kupata fedha nyingi kwa haraka lakini kirahisi, ni mara chache sana utamkuta anafanya kazi halali.

Uovu mwingi umejificha katika kupenda fedha. Mwanamke apendaye fedha ni muovu na ni mchafu, unaweza kumuona kama vile ni mwema lakini yuko tayari kuutoa uhai wako ili apate fedha uliyonayo. Mwili wake ataufanya kuwa ni bidhaa ili apate fedha.

Mwanamke apendaye fedha yeye huangalia tu mwanaume wenye fedha ili aweze kuolewa naye. Kiuhalisia hampendi yule mwanaume bali anapenda fedha yake. Na wanawake wengi wenye sifa hii ya kupenda fedha huwa wavivu wa kufanya kazi na kama wanafanya basi ni kazi zisizojulikana, hutanguliza maslahi yao kwanza, na fedha kwao huwa kipaumbele cha kwanza kabisa, na tafsiri ya upendo kwao ni wao kupewa fedha na wapenzi wao au wenzi wao. Usipompa fedha maana yake humpendi, na kama utakuwa huna fedha za kumpa kwake utakuwa huna maana kabisa. Wanawake wa aina hii hawawezi kuolewa, au huolewa kisha wakaachika kwa sababu huwa tatizo ndani ya ndoa.

Wanawake wa tabia hii wana mahusiano na fedha ya mtu lakini hawana mahusiano na yule mtu anayemiliki fedha zile. Fedha ikiisha na mahusiano ndio yanafikia mwisho. Wanaume wengi wenye akili kwa kujua hilo, kwa sababu wana nia na dhamira safi ya kuoa na kuwa na mke wa maisha yao yote, huwakwepa wanawake wa namna hii. Wanatafuta wanawake ambao watakaa nao maisha yao yote katika shida na raha.

Wanawake wenye kupenda fedha hawataki shida, wanataka raha tu na kwao pesa ndio raha na si kitu kingine. Wanawake wa tabia hii huwa hawadumu katika mahusiano na huwa ni miiba katika mahusiano, na Mungu hawezi kuwapa mume, ni mwanaume mjinga tu ndiye atakayenasa katika mtego wao.

Tabia Namba Nne. UVIVU

Mithali 20:14

Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu.​

Uvivu ni mzigo kwa aliyenao, na mtu mvivu ni mzigo kwa watu waliyenaye na wanaomzunguka. Uvivu ni hasara kabla ya kupata hasara; uvivu unakufanya upate hasara kabla hata hujafanya kitu ukapata hasara kwa sababu hutafanya kabisa kitu. Kutokufanya kitu kabisa ndio hasara kubwa ulimwenguni kuliko ile hasara unayoipata baada ya kufanya kitu.

Mithali 19:15 inasema, Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito, na Mithali 26:14 inasema, Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake, kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake. Kitandani ni mahali ambapo mtu hujilaza ili apate usingizi, na mvivu hupenda sana kitanda kwa sababu uvivu wake humtia katika usingizi mzito.

Mwanamke mvivu ukitaka kumjua mwangalie anaamka saa ngapi, na katika kutwa nzima analala mara ngapi. Biblia inatufundisha kwamba mke mwema hutangulia kuamka mapema kabla ya mapambazuko ili afanye kazi zake na kuwapangia wengine kazi za kufanya waliomo nyumbani mwake, lakini pia huamka mapema kumwandalia mumewe chakula na mazingira mazuri ya kwenda kazini kwake. Huamka kabla ya mumewe kuamka, yeye anakuwa wa kwanza kutoka kitandani (Soma Mithali 31:10 – 31).

Lakini kwa upande wa mwanamke mvivu mumewe ndiye huamka mapema na kuanza pengine kumwamsha yeye, au pengine huondoka hadi kwenda kazini mkewe akiwa bado amelala na wala hajui mumewe kaondoka na amevaa nguo gani, ameoga au hajaoga, na huku nyuma huamka saa tano asubuhi.

Binti mvivu huwahi kupanda kitandani na huchelewa kutoka kitandani, kitanda ni rafiki yake wa karibu sana na usingizi ni mwenzi wake wa dhati kweli. Kila wakati ni yeye anataka kulala, kama hutamkuta kwenye televisheni akiangalia tamthilia basi utamkuta kitandani kalala, au sebuleni kwenye kochi na simu yake akichati; ni mbaya sana, na mwanamke wa namna hii hawezi kuolewa na hata kama akiolewa ndoa yake itakuwa na shida.

Mithali 6:9, anamuuliza swali mtu mvivu, anasema, Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka hata lini katika usingizi wako? Usingizi sio tu kulala kitandani, lakini pia usingizi ni pamoja na wewe kukaa bila kufanya kazi yoyote. Ni wewe kukaa kizembe zembe bila kujishughulisha na chochote ukisubiri kuolewa. Hii ni tabia hatarishi sana ambayo inahatarisha mahusiano yako ya uchumba na ndoa.

Mtu ambaye hafanyi kazi, amekaa tu, huyo amelala, yupo usingizini, na kwa sababu ni mvivu anafurahia huko kulala na huo usingizi alionao. Na kwa sababu mtu aliyelala usingizi huwa hasikii wala kuona mambo yanayoendelea katika dunia hii, hupitwa na mambo mengi bila hata ya kujua na hufanya mambo mengi yasiyo na maana bila hata ya kujua anafanya nini kwa sababu yupo usingizini. Kile anachoweza kufanya usingizini ni kuota ndoto za mambo mazuri anayoyatamani lakini si vitu halisia katika maisha yake, ni njozi tu. Kwenye njozi anaishi maisha mazuri lakini kwenye ulimwengu halisi anaishi maisha yasiyo yake.

Mwanamke mvivu ni jipu na linapaswa kutumbuliwa, jipu likiwa ubavuni pako mwili wako hautakuwa na raha kabisa, kuliko kuwa na jipu ubavuni mwako, kuliko kuwa na mwiba ubavuni mwako ni bora kutokuoa kabisa. Mwanmke kama unataka ndoa yako iwe safi, acha uvivu chapa kazi.

Tabia Ya Tano: DHARAU NA KIBURI

Mithali 22:10

Mtupe mwenye dharau, na ugomvi utakoma; Naam fitina na fedheha zitakoma.​

Mwenye dharahu husababisha ugomvi kwa sababu ndani yake kuna fitina na fedheha. Dharahu ni matokeo ya kiburi na huleta ugomvi baina ya watu. Dharau ni kukosa heshima na adamu mbele za watu, ni kuwakosea watu heshima na adabu, ni kuwaona wao hawafai ila wewe peke yako ndiye unafaa. Ni kuwashusha watu chini ya miguu yako na kuwakanyaga.

Mwanamke mwenye dharau hawezi daima kuolewa kwa sababu dawa ya kuepuka ugomvi, fitina na fedheha ni kumtupa nje mwenye dharau. Hakuna mtu anayependa dharau, na kama kuna kitu wanaume hawakipendi maishani mwao na wanakiogopa sana ni kudharauliwa kwa jambo lolote lile kwa maneno au kwa matendo.

Wanawake kwa sababu ya ile hali ya kiburi (cha uzuri wao) huwa na dharau sana hasa pale anapojiona yeye ni mzuri sana na ni bora kuliko wengine na kuanza kuutumainia uzuri wake. Pale anapoona kila mwanaume anavutika na uzuri wa sura na umbo lake ndipo hujisahau na kuanza kuota kiburi kwa sababu ya uzuri wake na dharau kuzaliwa. Ni kweli wanaume wengi watakuja kwako, lakini watakuja na kuondoka bila kukuoa kwa sababu watakutana na kitu wasichokipenda, nacho ni kiburi na dharau.


 đź‘‰đź‘‰Mwanaume akija kwako na akakaa ni kwa sababu ya tabia na si maumbile yako. Hapo naomba ulielewe na liingie akilini mwako kabisa.


Mithali 29:8 inasema, Watu wenye dharau huwasha mji moto; Bali wenye hekima hugeuza mbali ghadhabu. Hakuna mwanaume anayependa mji wake uwashwe moto, kila mwanaume anapenda usalama ndani ya mji wake. Mwanamke mwenye dharau huwasha moto ndani ya mji, kwa sababu ya dharau yake kila mumewe anapokuja nyumbani hakukosi kuwa na ugomvi na mapigano kwa sababu maneno na matendo yake mwanamke huyu huchochea hasira ya mumewe. Kwa sababu wanaume ni waoga sana wa kuzozana, huishia kuwapiga wake zao au kuikimbia nyumba kwa sababu inawaka moto.

Dharau ni kiberiti husababisha moto, na kwa kuwa hakuna anayependa kuungua mwanamke mwenye dharau atakimbiwa na wanaume wenye heshima. Hakuna mwanaume mwenye heshima atakayekubali kuoa mwanamke mwenye dharau na kiburi, yaani hakuna kabisa. Kwa hiyo kiburi ni tabia hatarishi sana kwa mwanamke si tu anayetaka kuolewa lakini pia na yule ambaye tayari yupo katika ndoa. Kwa nini? Kwa sababu mumeo anahitaji heshima yako kwake ili ajisikie salama kuwa karibu yako, la sivyo atakuwa anawahi kuondoka nyumbani na anachelewa kurudi nyumbani kama sio, kutokurudi kabisa.

Yafikiri hayo, lakini tukumbuke kuwa hizi ni  nyakati za mwisho, kanisa la Mungu tujipange kwa ajili ya kuondoka.

Mungu akubariki sana

Kuendelea kuelewa bofya link hii hapa👇

https://youtu.be/nnYXfxwGSpk

Taifa Teule Ministry

0628187291 / 0744474230

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI