NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?
NINI MAANA YA KUTOKA KATIKA MADHEHEBU?
Mimi ni Mathayo Sudai, karibu tujifunze jambo hapa leo.
Kwanza jambo la kufahamu ni kwamba kila mkristo anapaswa awe na Roho Mtakatifu, ambaye kwa huyo biblia inasema ATATUONGOZA NA KUTUTIA KATIKA KWELI YOTE.
Yohana 16: 13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake”.
Hivyo mtu yeyote asiyekuwa na Roho wa Mungu biblia inasema huyo si wake (Warumi 8:9), Haiwezekani kumjua Mungu kwa namna yoyote ile,. Sasa tatizo linatokea ni pale unakuta watu wengi walipokea kweli Roho Mtakatifu mwanzoni walipoamini, lakini ilifikia wakati Fulani wakamzimisha pasipo hata wao kujijua, Uthibitisho ni kwamba utasikia mtu anakwambia mwanzoni nilipompa Bwana maisha yangu nilikuwa ni moto sana, lakini siku hizi nimepoa, ile nguvu ya mwanzo sina..sasa hiyo ni dalili ya awali kabisa ya mtu aliyemzimisha Roho ndani yake, biblia inasema, katika (1Wathesalonike 5: 19 MSIMZIMISHE ROHO; )
Unaweza ukaona hapo, Roho wa Mungu anaweza kuzimishwa, na anazimishwa kwenye nini?, ,Jibu ni kwamba anazimishwa katika eneo la kuendelea kukuongoza katika kweli yote.. Na madhara ya kutofikia kile kiwango kinachohitajika na Mungu ni kukaa katika hali hiyo hiyo ya kutokuwa na ufahamu wa kutosha kumuhusu Mungu,hivyo ni rahisi kudanganywa na kuchukuliwa na mafundisho mengi ya uongo, unakuwa ni kama unyasi unaotikiswa na upepo.
Sasa njia pekee inayowasababisha wengi wamzimishe Roho ni UDINI na UDHEHEBU, Kwa mfano wakati Bwana Yesu alipokuwa duniani, aliwakuta watu wakiwa katika dini zao na madhehebu yao, nao si wengine zaidi ya mafarisayo na masadukayo, Hawa watu sio kwamba walikuwa ni wabaya sana, hapana, kwanza vitu vingi walivyokuwa wanashika yalikuwa ni maagizo ya Mungu, na walikuwa wanafanya bidii kweli katika kuvishika na kuvisimamia, lakini torati waliyokuwa wanaishika haikuwa imekamilika, na alipokuja Bwana kuwaeletea habari ya kuitimiliza torati, walimpinga na kumkataa, lakini ni kwasababu gani?, sababu ilikuwa si nyingine zaidi ya kujikinai katika Dini zao na udhehebu wao. Na kukataa kumruhusu Roho Mtakatifu awafundishe zaidi na kuwatia katika kweli yote…
Sasa matokeo yake wakaukosa uzima waliokuwa wanautazamia na kupelekea kugeuka kuwa wapinga-Kristo badala yake. Kwasababu walihama kabisa katika kuongozwa na Roho wakaenda katika kuongozwa na dini, na taratibu za madhehebu yao..Pengine walianza kusema dhehebu letu ndio la zamani na la kipekee, lina watu wengi, tuna masinagogi mengi duniani kote,..Tunaheshimika na mataifa yote, tuna wasomi wengi, tunafadhili miradi mingi ya kijamii, tunaongoza katika kusaidia maskini na yatima,..Sasa huyu mtu anayejiita YESU, na Yohana Mbatizaji wanatuletea habari za ubatizo wa maji, wanazitolea wapi? Mambo hayo hayapo kwenye torati, kwanza ni watu wa kawaida, wanatafuta wafuasi,..Lakini Bwana Yesu aliwaambia kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu, Yohana 3:5 ”….Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.”
Sasa wao walibakia tu katika sheria za dini na madhehebu, kwamba usipotahiriwa huwezi kumwona Mungu,
Kadhalika na katika wakati huu wa sasa, hakuna mahali popote Mungu alianzisha dhehebu, sisi wote kwa pamoja ni wakristo, na mikusanyiko yote yanapaswa yawe na imani moja, ubatizo mmoja na Roho mmoja, Bwana mmoja, Mungu mmoja, (Waefeso 4:4-5), lakini hiyo imekuwa ni tofauti katika kanisa la leo, imani ni nyingi tofauti tofauti, batizo ni nyingi tofuati tofuati, na kibaya zaidi ni kwamba kila mmoja anaamini cha kwake ndio sahihi,..wengine wanasema sisi ni wa Luther, wengine wanasema sisi ni wa Branham, wengine wanasema sisi ni wa Hellen White, wengine wanasema sisi ni wa John Wesley, n.k… Lakini Mtume Paulo baada ya kuliona jambo kama hilo la kanisa kugawanyika vipande vipande katika madhehebu alisema hivi…
1Wakorintho 1: 12 Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.
13 Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?
Unaona hapo? Kanisa la Kristo haligawanyiki kwasababu Kristo hajagawanyika, tungepaswa wote tunapokusanyika wote tunakuwa ni ndugu katika Imani moja. Sasa inapotokea Roho wa Mungu anapotaka kumwongoza mtu katika kuijua kweli zaidi, labda tuseme anamfundisha juu ya ubatizo sahihi ya kwamba anapaswa akazamishwe kwenye maji mengi, na kwa jina la YESU KRISTO,. Lakini mtu Yule mtu badala ya kuchunguza maandiko na kumwomba Roho Mtakatifu amsaidie, moja kwa moja atakwenda katika dhehebu lake, je! Wanaamini hivyo?, akikuta dhehebu lake hawaamini hivyo, basi na yeye analitupilia mbali. Hajui kwamba ameshamzimisha Roho pasipo hata yeye kujijua, na watu wa namna hiyo ukitazama maisha yao ya kiroho yanakuwa ni chini siku zote, na mwisho wa siku wanageuka kuwa wapinga-kristo kama walivyokuwa mafarisayo na masadukayo, kwa jambo dogo tu la udhehebu na udini. Wanaanza kuwapinga vikali wale wote wanaofundisha kinyume na mapokea yao.
Tukiyajua hayo sasa, biblia inaposema “TOKENI KWAKE ENYI WATU WANGU” (Ufunuo 18:4), haimaanishi kutoka kwa miguu, bali ni katika roho, na ufahamu, ni kutoka katika kamba za dini na madhehebu, kutoka katika makosa yaliyofanywa, kutokufungwa na mifumo ya dini na madhehebu inatakayokufanya usipige hatua moja ya kiroho (huko ndiko kumzimisha Roho).. Unapoona kweli sehemu Fulani inafundishwa, usikimbilie kulinganisha na dhehebu lako au dini yako inasemaje juu ya hilo..moja kwa moja kimbilia kulilinganisha na Neno la Mungu, hapo ndipo Roho Mtakatifu anaanza kupata nafasi ya kukufundisha na kukuongoza katika kweli yote…
Kwa mfano umesikia mahali unafundishwa ibada za sanamu ni machukizo mbele za Mungu, lakini katika dhehebu lako ni jambo ambalo mmekuwa mkilifanya siku zote. Sanamu imekuwa ni sehemu ya ibada zenu, sasa ili usimzimishe Roho, usikimbilie kwenda kuangalia dhehebu lako linasemaje, wewe kimbilia kuangalia Neno la Mungu linasemaje juu ya hilo, ndio Roho Mtakatifu unakuta anakuongoza katika huu mstari..
2Wakoritho 6: 15 “Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
16 Tena pana mapatano gani kati ya HEKALU LA MUNGU, na SANAMU? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
17 KWA HIYO, TOKENI KATI YAO, MKATENGWE NAO, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.
18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”
Sasa ukishalifahamu hilo kwa usalama wa Roho yako, unapaswa uondoke hapo, utafute sehemu nyingine ambayo sanamu haichanganywi na ibada tukufu ya Mungu…kadhalika na mambo mengine kama hayo, kwa jinsi utakavyompa Roho Mtakatifu nafasi atakuwa anakuongoza katika kweli yote mpaka unafikia kimo cha mtu mkamilifu mbele za Mungu.
Kwahiyo unapokaa katika mkusanyiko wowote unaojiita ni wa Kikristo, chunguza ni vipi vinavyoendana na Neno la Mungu, ndivyo ushirikiane navyo, na vile visivyotokana na Neno, jitenge navyo tena mbali sana. Uongozo wako uwe ni BIBLIA na hapo ndipo Roho Mtakatifu atakapotumia kukuongozea.
Pia ni muhimu kukumbuka madhehebu ndiyo yatakayokuja kuunda ile chapa ya mnyama huko mbeleni..kwahiyo ni kuwa makini sana. Kadhalika katika siku za mwisho Bwana Yesu alisema kutakuwa na makundi mawili ya wakristo,. Kundi la kwanza linajulikana kama wanawali wapumbavu na la pili kama wanawali werevu (Mathayo 25). Ukisoma pale utaona Wale werevu walibeba Taa pamoja na mafuta yao ya ziada wakati wa kwenda kumlaki Bwana wao, lakini wale wapumbavu hawakubeba mafuta ya ziada, na wakati Bwana wao alipokaribia kuja taa zao zikaanza kuzima, kwasababu hawakuwa na mafuta ya ziada, hivyo hawakufanikiwa kuingia katika karamu ya Bwana wao japo nao walikuwa wanamngojea Bwana wao..
Lakini wale wanawali werevu wanawawakilisha wakristo waliopokea Roho Mtakatifu na kwasababu ni werevu hawakuridhika na mafuta waliyonayo machache, walitembea na mafuta mengine ya ziada ambayo yanawakilisha ufunuo na mafundisho ya Roho Mtakatifu hivyo mpaka Bwana alipokuja wakakutwa taa zao bado zinawaka, na ndipo wakaenda naye karamuni (huko ndiko kutokumzimisha Roho). Lakini wale wapumbavu ni wakristo ambao baada ya kumpa Bwana maisha yao, wakaridhika tu katika mapokeo ya dini zao na madhehebu yao, na siku Bwana atakapokuja atawakuta katika hali hiyo ya uvuguvugu, kuzimika kwa taa zao (kwasababu walishamzimisha Roho Mtakatifu zamani)..Hivyo watatupwa katika lile giza la nje, ambalo hilo linawakilisha dhiki kuu na ziwa la moto.
Hivyo ndugu unaona madhara ya kutotembea na Roho Mtakatifu katika safari yako ya ukristo? anza sasa kumruhusu Roho atende kazi ndani yako, toka katika kamba za dini na madhehebu, dumu katika Neno ili Mungu akufikishe mahali alipokusudia ufike. Kumbuka, Yesu ni mmoja, ubatizo ni mmoja, Roho ni mmoja.
Ubarikiwe sana.
Kwa maswali na chochote usichokielewa, pamoja na wote wenye shida mbalimbali kwa maombezi, na kama hujabatizwa bado unahitaji kubatizwa, au hujaokoka unatamani kumpa Bwana maisha leo, wasiliana nami
0655891197/0628187291
Maoni
Chapisha Maoni