JE NI DHAMBI KULA NYAMA SIKU YA IJUMAA KUU

NI DHAMBI KULA NYAMA SIKU YA IJUMAA KUU ?



Mimi ni Mathayo Sudai.  Ungana nami katika uchambuzi huu wa mapokeo ya ijumaa kuu.
Ili iwe vyepesi kwetu kulielewa vizuri somo hili. Tutajifunza somo hili kwa kuligawa katika vipengele viwili. Ambavyo ni:-


1.KWANINI WAKATOLIKI HAWALI NYAMA SIKU YA IJUMAA KUU?

2.UCHAMBUZI WA HOJA 4 KI-BIBLIA KUHUSU MAPOKEO YA KANISA CATHOLIC.


UTANGULIZI


Leo ni siku ya Ijumaa Kuu. Inaitwa siku ya ijumaa kuu kwa sababu ndiyo siku ambayo Wakristo wote kote duniani wanaadhimisha kumbukumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo msalabani kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima.


Utasikia kwenye vyombo vya habari eti wanasema:- "......Wakristo leo wanakumbuka mateso ya Yesu kristo mwokozi wao........ Wakristo wanasherekea kufufuka kwa Yesu mwokozi wao......................................"


Matamshi hayo ndani yake yamefichwa na hila fulani za shetani. Ni muhimu kuelewa vizuri hapa, Yesu Kristo hakuteseka na kufa tu kwa ajili ya wakristo wala yeye sio mwokozi wa wakristo. La hasha! Bali YESU NI MWOKOZI WA ULIMWENGU MZIMA, yeye alijitoa nafsi yake kuwa sadaka ya ukombozi kwa ajili ya kila mwanadamu mwenye mwili hapa duniani. Yeye sio mwokozi wa wakristo tu bali yeye ni MWOKOZI WA ULIMWENGU. Neno la Mungu linasema katika

YOHANA 3:16-18:-"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye (Katika ulimwengu) asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, BALI ULIMWENGU UOKOLEWE KATIKA YEYE. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu."


YOHANA 4:42:-"..........Maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa HAKIKA HUYU (YESU) NDIYE MWOKOZI WA ULIMWENGU".


Haijalishi kwamba mtu huyo anamwamini au hamwamini Yesu, anamkubali au anampinga. Vyovyote vile iwavyo, bado hakuna ukombozi mwingine nje na Bwana Yesu, na tena MWANADAMU HASAMEHEWI DHAMBI ZAKE BILA KUMWAMINI YESU. Maana hapa duniani hakuna jina jingine walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa ni jina la Yesu Pekee yake. Tena Yesu ndiye NJIA, KWELI na UZIMA. Mtu akiamua kumuacha Yesu na kwenda kwenye dini nyingine, ni hakika amedanganyika na kupotea gizani kabisa. Ni mjinga na kipofu wa kiroho. Ni kwa sababu yeye anayemkosa Yesu ndani yake amekosa huo uzima, hujidhuru nafsi yake mwenyewe na kwenda kwenye mauti ya milele-Jehanamu ya moto

[YOHANA 14:6; MATENDO 4:12; LUKA 24:46-47; WARUMI 3:23-26; MITHALI 8:35-36]. Huo ndio ukweli hakika usiyopindishwa.


Baada ya kufahamu hayo. Turudi kwenye mada yetu ya msingi ya somo letu. Wako wakristo na baadhi ya watu wengine ambao wanauliza habari ya kula nyama siku ya ijumaa kuu kwamba ni dhambi kweli? Na hili jambo likoje ki-biblia? Maana kuna matangazo yamezagaa kila mahali yakizungumzia wakristo kutokula nyama siku ya ijumaa kuu.


Watu wanapenda kuufahamu ukweli huu ukoje hasa ki-biblia? Nami nimeona nilete ufafanuzi wa somo hili ili tuifahamu kweli na hiyo kweli ituweke huru. Maana Biblia inasema katika YOHANA 8:31-32:-"Basi Yesu akawaambia wale wayahudi waliomwamini, NINYI MKIKAA KATIKA NENO LANGU, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena MTAIFAHAM KWELI, NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU".


Sasa kweli hiyo ya kutuweka huru ni nini? Biblia inaendelea kusema katika YOHANA 17:17:-" Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli".


Neno la Mungu ndio kweli na sio mapokeo ya wanadamu. Yesu hakusema mkikaa katika mapokeo ya dini yako utakuwa mwanafunzi wangu kweli kweli. Hapana! Bali alisema NINYI MKIKAA KATIKA NENO LANGU mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Sasa neno la Mungu (Biblia) ambalo ndiyo neno la Yesu, limetufundisha nini kuhusu suala la kutokula nyama siku ya ijumaa kuu? Kuna mahali popote tumekatazwa katika Biblia?

Kabla ya kwenda huko ni vema kwanza tuelewe juu ya:


1. KIPENGELE CHA KWANZA

KWANINI WAKATOLIKI HAWALI NYAMA SIKU YA IJUMAA KUU?


Wao wanaeleza hivi:-
"Katika jamii nyingi, nyama ni miongoni mwa vyakula vya starehe. Ndivyo inavyoaminika kwa watu wengi. Hivyo, hapana budi kujua kuwa, maana ya msingi ya kutokula nyama katika Ijumaa Kuu, ni moja tu, kufunga starehe. Ijumaa Kuu ni siku ya mateso na kifo cha Yesu Kristo.

Katika mazungumzo na Katibu Mtendaji (Mkuu) wa Idara ya Liturjia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Paul Chiwangu alisema kwa Mkristo Mkatoliki, kula nyama katika Ijumaa Kuu ni dhambi maana Kanisa linahimiza kujinyima siku hii ili kuyakumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo.
Katika moja ya machapisho ya gazeti la Kiongozi linalomilikiwa na TEC, Padri Titus Amigu aliwahi kuandika akisema, “Mateso hadi kifo cha Yesu msalabani, yamempata kutokana na dhambi zetu hivyo nasi tunakusudia kuacha starehe zetu na tunafunga ili tujutie dhambi zetu.”


“Hii ni kusema kuwa, tunafunga ili tutubu dhambi zetu na Mungu atuonee huruma na kutusamehe dhambi zetu na wengine ambao ni wadhambi kama sisi maana, kufunga, ni mapambano baina yetu na dhambi pamoja na mkuu wa dhambi yaani shetani.”

Injili ya Marko 6:26 inasema kwamba, katika kesi na masuala fulani, shetani hatoki pasipo sala na kufunga. Padri Amigu anaandika kuwa, katika suala la kufunga, inampasa mtu kuchagua kitu kizuri cha kukiacha.

Anasema, “Kwa mfano, huwezi kufunga kitu kama kula ugali wa muhogo wakati ugali wa namna hiyo kwako ni shida, bali unafunga kitu kizuri kama labda kula wali na pilau. Huko ndiko kweli kufunga, kujikatalia na kujitesa kwa toba.”


Akaongeza: “Ieleweke kuwa, tangu enzi zile za kale, huko ilikoanzia dini yetu na huko kulikoanzia kufunga, waamini waliacha kula nyama na vitu vitokanavyo kama vile siagi na maziwa kwa vile vilikuwa ni vitu vinavyochukuliwa na kueleweka kuwa ni vya anasa na vile vilivyowakilisha anasa vilipopatikana.”

Hilo, ndilo tulilolipokea kutoka kwa wamisionari kwamba, tunapofunga tuache kuvitumia vitu vya anasa na starehe; nyama ikiwa kitu kimojawapo.”

Kimsingi, kwa vile vitu vya starehe hapa duniani sio nyama pekee yake, kila mwamini anaalikwa kukagua vitu vyake vya starehe na hivyo, navyo tuviache siku ya kufunga apate muda zaidi wa kuhuzunika na dhambi zetu tukiomba toba kwa Yesu Kristo aliyesulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu.
Kadhalika, katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya, Padre Amigu aliyekuwa Mkuu wa Seminari Kuu ya Peramiho Jimbo Kuu Katoliki la Songea, alisisitiza kuwa, mbali na sababu za kiimani katika dini, pia ipo sababu nyingine ya kibinafsi inayowafanya watu wengine wafunge kula nyama siku kama ya leo.

Akasema, “Hii ni ile sababu ya kufananisha nyama ya kuliwa na mwili au nyama ya Yesu Kristo aliyepigwa mijeledi na kutobolewa na kuchubuliwa na kuachwa akivuja damu nyingi. Hii ni hali inayowafanya wengine, washindwe kula nyama wakiona maiti ya mtu yeyote.”

Akasisitiza kuwa, hii ni sababu ya kibinafsi kwa kuwa Kanisa linapowasisitiza waamini kufunga kula nyama katika Ijumaa Kuu, lina hoja moja kubwa na ya msingi, ile ya kuacha starehe na kufunga na, siyo hiyo nyingine ya kuona nyama kama kitu kinachofanana na nyama au mwili wa Yesu Kristo ambayo kimsingi haina nguvu.

Kwa msingi huo katika Ijumaa Kuu pamoja na kuacha kula nyama tuache na starehe zetu, mambo yanayotuvutia ili tukumbuke dhambi zetu na kutubu toba ya dhati inayotoka ndani ya moyo.

2. KIPENGELE CHA PILI

UCHAMBUZI WA HOJA 4 KI-BIBLIA KUHUSU MAPOKEO YA KANISA CATHOLIC

Nimuhimu kuelewa na kufahamu kwamba:-

(1) Kutokula nyama siku ya ijumaa kuu ni mapokeo ya kanisa Catholic tu na SIO AGIZO LA BIBLIA.

Neno la Mungu wetu linatuambia katika WAKOLOSAI 2:8, 20-23:-" Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwanini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Mshike, msionje, msiguse; (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo huonekana kuwa yana hekima, KATIKA NAMNA YA IBADA MLIYOJITUNGIA WENYEWE, na katika kunyenyekea, nay katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili".

Kama wapendekoste yaani watoto wote wa Mungu tuliokolewa hatupaswi kuwa na hofu yoyote wala tusifuate mkumbo wa kiimani wa kutokula nyama siku ya ijumaa kuu kama wengine walivyodanganyika wakidhani ni agizo la Mungu au mapenzi ya Mungu kufanya hivyo. Kumbe siyo! Bali ni mapokeo tu ya dhehebu lao katika desturi na ibada waliojitungia wao wenyewe tu na sio agizo la Mungu.


(2) Kanisa la kweli la Mungu hatupaswi kuongozwa na mapokeo yetu ya kidini, bali tunaongozwa na Neno la Mungu (Biblia).


ZABURI 119:9,105:-"Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata Neno lako. Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia zangu".

2 TIMOTHEO 3:16-17:-" KILA ANDIKO , LENYE PUMZI YA MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na katika kuwaadibisha watu katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema".

Na kwa msingi huo hakuna andiko lolote katika Biblia linalotuagiza au kutufundisha au kutukataza kula nyama siku ya ijumaa kuu au siku yoyote nyingine. Kama nilivyotanguliza kusema na kufafanua hayo ni mapokeo ya kidini ya watu wao walivyopokeana wao kwa wao na wala sio agizo la Neno la Mungu, kama ilivyoandikwa.

Hivyo hatupaswi kubabaika. Ukiamua na ukipenda wewe kula nyama tu kwa sana siku ya ijumaa kuu Leo . Biblia imeturuhusu kula vyote wakati wowote bila kuuliza-Uliza. Kama siku ya leo umekuta sehemu wamepika nyama, wakikukaribisha, WEWE KULA KWA SANA TU, Yanini kujitia chini ya sheria za mapokeo ya kidini akati sio neno la Mungu! Wewe vuta saani hilo, jinomeneshe kwa raha zako zote.

Biblia inasema katika 1WAKORINTO 10:25-27, 30-31:-"KILA KITU KIUZACHO SOKONI KULENI, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri; maana , Dunia ni Mali ya Bwana na vyote viijazavyo. Na mtu asiyeamini akiwaalika, nanyi mnataka kwenda, KULENI KILA KITU KIWEKACHO MBELE YENU BILA KUULIZA-ULIZA, kwa ajili ya dhamiri. Ikiwa Mimi natumia sehemu yangu kwa shukrani, kwanini nitukanwe, kwa ajili ya kitu nikishuriacho? Basi mlapo, au mnywapo au mtendapo neno lolote , fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu".


Ndugu yangu mpendwa msomaji unaweza kuona mpaka hapo, hahahaha! Hilo ndilo neno halisi la Mungu linavyotufundisha na kutuagiza kufanya na wala sio vinginevyo.


(3) Anayekula nyama siku ya ijumaa kuu na yule asiyekula, wote hawana kosa/dhambi yoyote juu ya hilo mbele za Mungu; la msingi tusikwazane wala kuhukumiana tu.


Ndivyo Neno lake Mungu linavyotuagiza ama kutufundisha. Biblia inasema juu ya hilo katika:- WARUMI 14:1-9, 13-22:-"Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimuhumu kwa mawazo yake. MTU MMOJA ANAYO IMANI ANAKULA VYOTE; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. YEYE ALAYE ASIMDHARAU HUYO ASIYEKULA, WALA YEYE ASIYEKULA ASIMUHUKUMU HUYO ALAYE; kwa maana Mungu amemkubali. Wewe u nani umuhukumuye mtumishi wa mwingine? kwa bwana wake mwenyewe husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. Mtu mmoja afanya tofauti kati ya Siku na siku; mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aiadhinishaye siku huiadhimisha kwa Bwana; NAYE ALAYE KWA BWANA, kwa maana amshukuru Mungu ; tena ASIYEKULA, HALI KWA BWANA, naye pia amshukuru Mungu. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwenu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake........."


1 WAKORINTO 8:8:-"Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu"


Neno la Mungu linachotufundisha hapo uamuzi wa kula nyama au Kutokula nyama inabakia kuwa ni hiyari ya mtu binafsi mwenyewe apendavyo. Hakuna sheria yoyote ya Mungu iliyotufunga juu ya hilo kwa habari ya siku. Ukipenda siku ya Leo ya ijumaa kuu kula nyama na usipopenda Acha. Na ukijilazimisha Leo kula nyama huku ndani ya moyo wako hupendi- huna amani kula, ni afadhali uache tu. Kwa maana ukila utakuwa umefanya dhambi. Kwa maana KILA TENDO LISILOTOKANA NA IMANI NI DHAMBI[ WARUMI 14:22-23]. Lakini kama ndani ya moyo wako huna mashaka yoyote una amani, wewe kula tu mpaka utoshoke. Na wala hakuna dhambi yoyote ile kwako mbele za Mungu .


(4) Kufunga ki-biblia siokuacha kula vyakula Fulani Fulani tu. La asha !


Ndugu zangu wakatoliki na watu wengine ambao wanashikilia mapokeo ya kibinadamu kama haya yasiyokuwa na mantiki wala sio jambo la kimaandiko, kama kipindi hiki cha ijumaa kuu mmeamua kukumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo kwa kufanya mfungo wa toba, mkiacha kula vile vyakula vizuri kama nyama n.k. Kama mlivyodai hivyo.
Niseme kwamba NI VEMA KABISA kipindi hichi cha kukumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo, kwa wewe ambaye unaishi maisha ya dhambi hujaokoka, au umeanguka kiroho, kufanya mfungo wa Toba [YOELI 2:12-13]. Lakini KUFUNGA KI-BIBLIA siokuacha kula vyakula fulani fulani tu aidha nyama, pilau n.k. La asha! Bali kufunga ki-biblia ni kuacha kabisa kula na kunywa chochote kile, siku nzima mchana na usiku [KUMBUKUMBU 9:18; ESTA 4:16; MATHAYO 4:1-2].

Na jambo hili halina mantiki kwa sababu.

1/Kwanini iwe ijumaa kuu tu wakati ukombozi huo ni endelevu?

2/Hakuna uhusiano wowote kati ya Damu ya Yesu na damu za wanyama.

3/Yesu Kristo mwenyewe alisema tuwe tunakula na kunywa chakula chenye kuleta picha na hisia za mwili na damu yake kila mara tunapokumbuka kufa kwake (Alitumia Divai na Mkate kama mfano halisi wa chakula). Hakuna mantiki yoyote kuzuia kula nyama kisa tu inaleta hisia za kuuwawa kwa Yesu.

4/Kifo cha Yesu kilikuwa ni jambo la kiroho, sasa kwanini leo wakristo wafungwe katika sheria za kimwili kama kutokula nyama?

Kumbuka pia

Neno "Kufunga" linatokana na neno la kiyunani "Nestevo", ambalo nalo linatokana na maneno mawili ya kiyunani "Ne" na "Esthio. Neno "Ne" maana yake "Bila" au "Hapana". Neno "Esthio" maana yake "Kula chakula au kinywaji". Neno "Nestevo" sasa linaunga maneno hayo mawili ya kiyunani "Ne" na "Esthio, na lina maana, "Bila kula chakula au kinywaji chochote". Hivyo, maana ya kufunga ni, "Bila kula chakula au kinywaji chochote". Kufunga sio kuacha kusoma gazeti tuliyozoea, kuacha kuchana nywele au kula chakulani fulani unachokipenda n.k. Nikuacha kabisa kula na kunywa kinywaji chochote. Maana hii ya kufunga inathibitishwa na maandiko yafuatayo:- EZRA 10:6; YONA 3:7; 2SAMWELI 3:35 ; ESTA 4:16; KUMBUKUMBU 9:9; MATENDO 9:9. Kufunga sio kuacha vyakula kama ugali, au wali halafu tunakunywa maji, soda, chai, maziwa, uji au kula matunda n.k. Ni kuacha kabisa kula chochote wala kunywa chochote kile. Huo ndio mfungo halisi wa ki-biblia, kama neno la Mungu linavyotufundisha.

Mungu awabariki wote kwa ujumbe wa neno hili.
Ukipenda kuwasiliana nami kwa ushauri , maombezi na mafundisho zaidi ya masomo ya neno la Mungu. 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI