TAWI LIZAALO HULISAFISHA ILI LIZIDI KUZAA

 TAWI LIZAALO HULISAFISHA ILI LIZIDI KUZAA 

Mimi ni Mathayo daudi sudai karibu katika ujumbe huu.

Yohana 15.1-7

 “1 Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.

 2 KILA TAWI NDANI YANGU LISILOZAA HULIONDOA; NA KILA TAWI LIZAALO HULISAFISHA, ILI LIZIDI KUZAA 

3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.

 4 Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.

 5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. 

6 Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.

 7 Ninyi mkikaa ndani yangu,”.


Kama wewe ni mkulima, au kama ulishawahi kujihusisha na shughuli yeyote ya kilimo, unaweza ukaelewa kwa undani uhusiano uliopo kati ya shina, matawi na matunda, utagundua kwamba mti hauwezi kuzaa matunda pasipokuwepo na shina, na kama shina halina matawi basi pia haliwezi kuzaa matunda. Kwahiyo ili matunda yawepo ni lazima liwepo shina pamoja na matawi.

Biblia inasema Bwana wetu Yesu Kristo ni mzabibu (shina), na Baba yake ndiye mkulima, na sisi ndio watu wake ndio matawi, kila tawi lisilozaa huliondoa na kila tawi lizaalo hulisafisha ili lizidi kuzaa.

Sentensi hii inaonyesha wazi kabisa huyu mkulima, yupo kwaajili ya kutafuta faida, yaani kupata matunda, utagundua kuwa sio mkulima wa kupanda tu na kuondoka bali utagundua ni mkulima ambaye yupo kimaslahi zaidi, na anafanya juu chini kuhakikisha anapata anachokitafuta.

Sasa ili kupata anachokitafuta ndio hapo tunaona anauchunguza mti wake siku baada ya siku kutafuta matawi yanayozaa ili aendelee kuyasafisha na yale yasiyozaa ayaondoe, na utaona hashughuliki na shina (yaani Yesu Kristo) bali utaona anashughulika na matawi (yaani wafuasi wa Yesu Kristo).

Sasa kama wewe ni mkulima utagundua kuwa ili kuufanya mti usiendelee kuwa mrefu kwenda juu huwa wanakata lile tawi la juu kabisa linalokua kwenda juu, na matokeo yake ni kwamba ule mti utaendelea kutanuka badala ya kuendelea kwenda juu, vivyo hivyo watu wakitaka mti uzidi kuwa mrefu kwenda juu, huwa wanaondoa yale matawi ya pembeni, na matokeo yake ule mti utaendelea kwenda juu sana lakini hautataanuka.


Kwanini wanafanya hivyo?..Ni kwasababu endapo yale matawi ya pembeni yakiachwa na kuendelea kuwepo ule mti hautaendelea kukua kwenda juu kwasababu nguvu yote au chakula chote cha ule mti kitaenda kwenye yale matawi yaliyopo pembeni na hivyo kudhoofisha ukuaji wa matawi ya juu, na vivyo hivyo kama wanataka mti upanuke kwa mapana, wanapaswa waondoe matawi ya juu ili chakula chote kisiende kwenye yale matawi yaliyopo juu na badala yake kiende kwenye yale matawi ya pembeni ili utanuke kwa kasi.


Kadhalika wakulima wa mazao ya biashara kama kahawa wanaelewa kwamba, wakitaka mmea kama mti wa kahawa uzae sana, huwa  wanakwenda kukata kile kikonyo cha juu kabisa cha mti wa mkahawa, ili usiendelee kwenda juu, na pia wanaondoa yale matawi madogo madogo ambayo yameota kwenye shina, ambayo hayazai, na kuacha yale matawi yenye matunda tu, na lengo la wao kufanya hivyo sio kwasababu hawapendi ule mkahawa uwe na matawi mengi, hapana! Bali wanajua endapo wakiyaacha yale matawi madogo yasiyozaa yaendelee kuwepo basi kuna hatari ya kuvuna kahawa chache kwasababu nguvu yote ya chakula badala iende kwenye yale matawi yanayozaa, inaishia kwenda kwenya yale matawi madogo madogo yasoyozaa, hivyo kusababisha matunda hafifu kutoka kwenye yale matawi makubwa yanayozaa. Hivyo utamkuta mkulima amekata matawi yote madogo madogo kama ni 20 au mia na kubakiwa tu na matawi matano au kumi makubwa yanayozaa.

Sasa hiyo hatua yote ya kupunguza matawi yasiyozaa ndiyo inayoitwa KUUSAFISHA MTI.

Sasa tukirudi kwenye ule mfano Bwana Yesu aliosema kwama kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa na lile lizaalo hulisafisha alikuwa ana maana kuwa, Kila mtu aliyekuwa ndani yake yeye asiyeonyesha dalili yote ya kuzaa matunda, Baba yake atamwondoa na sababu ya kumwondoa sio kwasababu anamchukia au hapendi awepo ndani ya Yesu Kristo, hapana!  Sababu pekee ya kumwondoa ni kwasababu ile nguvu au kile chakula ambacho kinatumika kwa mtu asiyezaa matunda kingeweza kutumika kwa mtu anayezaa matunda ili azae mengi zaidi na zaidi. Na ndio maana mahali pengine Bwana Yesu alisema..


Mathayo 25.29 “Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa”.


Nilikutana na ndugu mmoja mwislamu wakati Fulani, nikamwambia Bwana Yesu alisema kuwa mwenye kitu atapewa lakini asiye na kitu atanyang’anywa hata kile alicho nacho, Yule ndugu alihuzunika sana kusikia ile sentensi, alisema kwanini iwe hivyo, sio vizuri? Ina maana kwamba Yesu hana upendo kwanini amnyang’anye Yule asiyekuwa nacho hata kile kidogo alichokuwa nacho?. Nikajaribu kumweleza kuwa Bwana Yesu hazungumzii mambo haya ya  mwilini bali ya rohoni lakini bado alihuzunika. hivyo ndivyo ilivyo kwamba Bwana yupo kwa ajili ya faida, anachotaka kutoka kwetu ni matunda, sio nyuso zetu!! Na tutakuja kuyaona hayo matunda ni yapi muda mfupi baadaye.


Kwahiyo utaona kuwa, kuna hatari kubwa sana ya kutokuzaa matunda, hatari hiyo ni kwamba ile Neema na Baraka za Mungu juu yako za kumzalia Mungu matunda zinaondolewa kwako na kupewa mtu mwingine anayezaa, ndio hapo utakuta mwanzoni ulikuwa una hamu sana ya kumtafuta Mungu ghafla ile hamu inakufa, anaenda kuongezewa Yule mtu ambaye alikuwa anaonyesha bidii kidogo, anaongezewa nguvu mara mbili zaidi ya kumtafuta Mungu, utaanza kuona ile nguvu ya kuomba ambayo ilikuwa ndani yako ulikuwa una uwezo wa kuomba hata nusu saa, ghafla unajikuta hamu yote ya kuomba imekufa unaacha anaenda kuongezewa Yule ambaye kwa unyofu wa moyo kila siku anajitahidi aombe angalau aombe nusu saa, anaongezewa nguvu anaanza kuomba lisaa, masaa au hata mkesha, ukiona umepoa ghafla  fahamu tu kuwa umeondolewa kutoka katika lile shina, au upo hatarini kuondolewa.


Sasa ni Matunda yapi Bwana anayoyahitaji kutoka kwenye mashina (yaani mimi na wewe)?


Matunda ambayo Bwana anayahitaji yanatoka katika kitabu cha


Wagalatia 5:22 -23

“22 Lakini TUNDA LA ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”


Unaona hayo ndio matunda Bwana anayoyahitaji kutoka kwetu, anategemea katika kipindi chote tunachokaa ndani yake yeye kama mzabibu mkuu, anategemea kutuona tunazaa, upendo ndani yetu, tunazaa fadhili, tunazaa utu wema, tunazaa upole, tunazaa kuwa na kiasi na uvumilivu, tunazaa amani..hata baadaye tuwahubirie wengine habari njema za wokovu.


Lakini atakapokuja na kutukuta hatuzai hayo matunda ya haki badala yake  tunazaa, kutokusamehe, tunazaa wivu, tunazaa uasherati, tunazaa matusi, tunazaa kutokujiheshimu, tunazaa kiburi, tunazaa kuupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu, na bado tunasema sisi ni wakristo tupo ndani yake, bado tunasema sisi ni matawi yake, nataka nikwambie ndugu Kristo hana matawi ya namna hiyo, hii Neema iliyopo na wewe leo inayokulilia ugeuke utubu ili uzae matunda ya haki,itaondolewa kwako na kupewa watu wengine waliostahili. Ndivyo biblia inavyosema..


Mathayo 3.8-9 

“8Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. 

9 Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa PENYE MASHINA YA MITI; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni”


Na pia inasema “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao HAPANA MTU ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO; Waebrani 12:14”


Itii sauti ya Roho wa Mungu leo inayokuambia utubu uache dhambi zako na umgeukie Muumba wako leo kwa moyo wako wote! Itafika wakati hutaisikia tena ndani yako,siku hiyo injili kwako itakuwa ni kama upuuzi tu!.. Hujawahi kukutana na mtu hata umwelezeje hataki kusikiliza injili?? itii sauti ya Mungu inayokuambia leo, uache uasherati!, Uache uvaaji mbaya kama wanawake wa ulimwengu huu wasiomjua Mungu, uache sigara na pombe!, uache usengenyaji Mtii Mungu leo, kisije hicho kidogo alichowekeza ndani yako akakiondoa na kumpa mwingine, acha kudanganyika kwamba utatubu tu siku moja!! Hakuna kitu kama hicho hiyo ni sauti ya shetani mwenyewe ikizungumza ndani yako. Na acha kuamini injili za kwamba Mungu ni upendo tu! Mungu ni upendo tu! Hawezi kutufanya chochote…Yeye mwenyewe kasema mara kadhaa na sio sehemu moja kwamba “yeye asiye nacho hata kile kidogo alicho nacho atanyang’anywa” ikiwa na maana kwamba hatakuachia hata hicho kimoja ulicho nacho..


Mathayo 25: 28-29 

28BASI, MNYANG’ANYENI TALANTA HIYO, MPENI YULE ALIYE NAZO TALANTA KUMI. 

29 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa”.


Je! Sentensi hiyo haikuogopeshi?? Tubu leo ukabatizwe upokee kipawa cha Roho Mtakatifu. Ili ufanyike Tawi lizaalo.


Bwana akubariki.

Maoni

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI