NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA .

 Mimi ni Mathayo daudi sudai.

karibu katika ufafanuzi wa maneno haya katika kitabu cha luka 11.

     NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA

ENDELEA

Luka 11:24-26

 “24 Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema,

25 Nitairudia nyumba yangu niliyotoka.

26 Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza”.


Ukitafakari vifungu hivyo, utagundua tabia kadha wa kadha za mapepo;


1) huwa wanatabia ya kwenda kuishi mahali pasipokuwa na maji;

Ni adui wa maji; Sasa ni lazima ujue sehemu isiyokuwa na maji ni ipi kiroho?,,,, Ni moyo mkavu, usiokuwa na chemchemi ibubujikayo maji ya uzima ndani yake, yaani Roho Mtakatifu..


Yohana 4:14 “walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele”.


Mtu yeyote asiyekuwa na Kristo ndani yake, tayari kwa namna moja au nyingine ndani yake  kuna  mapepo, kwasababu ni kukame. Kwa urefu wa  habari hiyo ,nitumie ujumbe nikutumie somo lake;


    2) Tabia ya pili ni kwamba, yapo mapepo mengi ambayo hayana makao, yanasubiria tu, kualikwa.

Ndio maana ukisoma hapo anasema, likirudi na kukuta nyumba yake imefagiliwa, linakwenda kutafuta mengine saba yaliyo maovu kuliko yeye.


Jiulize linakwenda kutafutia wapi,? Hiyo ni kuonyesha kuwa yapo mahali fulani yanangojea kuitwa, na kwanini lisitafute limoja tu, bali saba? Ni kuonyesha kuwa yapo mengi, na kwanini lisitafute la saizi yake, bali yenye nguvu kuliko yeye. Ni kuonyesha kuwa na yenyewe huwa yanafanya uchaguzi, ni nani wa kukaa nao. Hiyo yote ni kujihakikishia ulinzi wake ili atakaporudi asibugudhiwe kwa lolote.


Kulithibitisha hilo, Soma ile habari ya Mariamu Magdalena, ambaye Bwana Yesu alimponya kwa kuyatoa mapepo saba ndani yake; Kuonyesha kuwa hapo kabla alikuwa ni mtu vuguvugu, yaani Mungu kidogo shetani kidogo, ndio maana yakamuingia yote yale kwa mpigo.


Marko 16:9 “Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba”.


Kuwa makini sana, unaposhiriki ibada yoyote ya Ki-Mungu, na ilihali maisha yako ni ya kipepo (yaani ya dhambi). Unazini, unalewa, unakwenda kwa waganga, unafanya anasa n.k. na wakati huo huo unakwenda kanisani kushiriki meza ya Bwana au kumwabudu Mungu, na kutoa sadaka.


Watu wengi leo hii hawajijui kuwa wanajiongezea tu idadi kubwa ya mapepo, kwasababu ibada yoyote uifanyayo kwa Mungu ni adui wa mapepo, hivyo yanapoona hali fulani ya hatari katika nyumba zao imetokea, Ni lazima yajihakikishie ulinzi kwa kuyaalika mengine saba yenye nguvu kuliko yenyewe.


Ndio hapo hali yako ya mwisho inakuwa mbaya kuliko ya mwanzo. Unakwenda kanisani, Neno limekuchoma, uache uasherati,  badala uache mambo hayo, unatoka kuendeleza tabia hizo, ujue kuwa utakuwa mzinzi mbaya kuliko hata ulivyokuwa pale mwanzo.


Ni heri ukatubu dhambi zako leo, Na kumfuata Bwana Yesu kwa kumaanisha kweli kweli, ufalme wa Mungu unapatikana kwa nguvu, biblia inasema hivyo, kwasababu shetani anajua kuwa muda wake ni mchache, hivyo anafanya kazi kwa bidii sana akishirikiana na mapepo yake, kuwaangusha watu.


Ndio maana siku hizi za mwisho hushangai kuona, maovu yamekithiri duniani, hata aibu tena hamna, hizo zote ni kazi za mapepo wachafu, ambazo  zimewavaa na kuwaendesha.


Hata wewe au mimi, tukiwa ni watu vuguvugu, hatueleweki tupo upande upi, tujue kuwa tupo kwenye hatari kubwa sana ya kuwa na mapepo wengi. Hivyo kwa haya machache ikiwa unataka, Kristo aanze na wewe upya katika maisha yako, na ayafukuze haya mapepo moja kwa moja.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI