DORKASI NI NANI KATIKA BIBLIA
Bwana Yesu asifiwe watu wa Mungu karibuni katika ujumbe huu kumtazama mwanamke aitwaye dorkasi
Matendo 9:36-37
“36 Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
Bwana Yesu asifiwe..
Ulishawahi kujiuliza kulikuwa na umuhimu gani, biblia kueleza tafsiri ya jina la mwanafunzi huyu aliyeitwa Tabitha?. Ukishaona mahali Fulani tafsiri ya jina la mtu inatolewa basi ujue kuna jambo Mungu anataka tujifunze, kwa huyo.
Mfano wa mtu mwingine kama Tabitha alikuwa ni Petro, Ukisoma Yohana 1:42, Bwana Yesu anafunua tafsiri ya jina lake.
Yohana 1:42 “Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).”
Unaona, kulikuwa na sababu ya Bwana kueleza tafsiri ya lile jina kwamba ni Jiwe/mwamba , ikiwa na maana kuwa zipo tabia, ambazo alikuwa nazo, au atakuja kuzionyesha zinazomwakilisha JIWE KUU mwenyewe ambaye ni Yesu Kristo..
Jambo hilo utalithibitisha mbeleni kidogo, katika Ufunuo alioupata kutoka kwa Mungu, kuhusiana na Bwana wetu Yesu Kristo, tusome;
Mathayo 16:15-19
“15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?
16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.
18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
19 Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni”.
Umeona akiwa anamaanisha kuwa juu ya mwamba(yaani Ufunuo alioupata kuhusiana na Yesu ni nani), ndio Bwana Yesu atalijengea kanisa lake hapo. Kwahiyo utaona kutolewa tafsiri ya jina lake tangu kule mwanzoni ni kwasababu ya matendo au funuo alizokuwa anazipata kuhusiana na Yesu Kristo, kama msingi wa Kanisa.
Sasa tukirudi kwa Tabitha naye, tafsiri ya jina lake linatolewa, kwamba ni PAA.
Paa, ni aina ya swala. Mwanzoni nilitafakari sana kwanini aitwe swala, asiitwe labda simba, au au kifaru, au dubu, majina yenye sifa, lakini badala yake anaitwa swala.
Je swala anatabia gani nzuri?
Swala ni mnyama ambaye ni mwepesi sana, miguu yake ipo haraka mno, na ni mwepesi wa kurudia juu, kiasi kwamba akikimbia, katika nyasi ndefu au uwanda tambarare, hata simba hawezi kumkamata, mnyama pekee porini ambaye anaweza kumkimbiza swala (Paa) Ni duma tu peke yake, tena kumpata kwake ni kwa shida sana.
Hivyo hiyo inamfanya, awe salama muda mwingi, akiwa porini.
Katika biblia mashujaa wa Bwana vitani walifananishwa na Paa, Kwamfano mmoja wa mashujaa wakuu wa Daudi aliyeitwa Asaheli alisifika kuwa mwepesi wa miguu kama swala hawa..
2Samweli 2:18 “Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu”.
“Kulungu, Paa, na Ayala” ni jamii hiyo hiyo moja ya Swala.
Soma pia,
1Nyakati 12:8 “Na wa Wagadi wakajitenga kumfuata Daudi ngomeni huko nyikani, waume mashujaa, watu waliozoea vita, walioweza kutumia ngao na mkuki; ambao nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, nao walikuwa wepesi kama kulungu juu ya milima;
Soma tena;
2Samweli 22:34-35
“34 Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.
35 Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu yaupinda upinde wa shaba”.
Wimbo 8:14 “Ukimbie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya manukato”.
Sasa mpaka hapo utapata picha ni kwanini Tabitha, aliitwa Paa, ni kwasababu miguu yake ilikuwa ni mepesi katika kutenda matendo mema. Mpaka akasifika katika mji mzima wa Lida, jinsi gani alikuwa tayari kwenda kuwashonea mitume nguo, na kanzu, Pamoja na watakatifu wengine,bila kuombwa wala kuulizwa, Jinsi gani alivyokuwa mwepesi wa kumtolea Mungu. Bila kusukumwa sukumwa, au kukumbushwa kumbushwa, yeye mwenyewe kama swala, alikimbia kutekeleza majukumu yake ya kiutumishi, Zaidi ya watu wote waliokuwa katika ule mji wa Lida.
Hatimaye akafa, lakini watu walimwona kama hastahili kuondoka mapema, watu waliliona pengo lake lilivyo kubwa, hadi wakati ule Petro, alipokwenda katika mji huo, kulikuwa na maiti nyingi lakini hakuitwa kwa mojawapo ya maiti hizo bali ya Dorkasi tu;
Matendo 9:36-40
“36 Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
38 Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu.
39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.
40 Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi”.
Hii ni kutufundisha kuwa, ili Mungu awe naye mwepesi kama Swala kutuhudumia, basi na sisi tuonyeshe wepesi wetu kwake. Je sisi nasi ni wepesi wa kutenda matendo mema kama Tabitha? Je tu wepesi kutoa mali zetu na vitu vyetu kwa ajili ya utumishi wa Bwana? Au tu wabinafsi, au mpaka tukumbushwe, au mpaka tulazimishwe, au mpaka tuvutwe vutwe?
Wakati mwingine kwanini, majibu ya maombi yetu yanachelewa?, Ni kwasababu sisi wenyewe sio wepesi kwa Bwana, tunamfanya yeye naye awe mzito.
Tuifanya miguu yetu mepesi, ili wakati wa haja zetu Bwana naye awe mwepesi kutusaidia, kama alivyofanya kwa Dorkasi.
Habakuki 3:19 “YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka”.
Mungu akubariki sana
Taifa Teule Ministry
Mwl /Ev Mathayo Sudai
0744474230 /0628187291
Aminaa sana Mtumishi wa MUNGU ubarikiwe Kwa ujumbe nzuri
JibuFuta