AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, ZINAZOCHUKIWA NA MUNGU

 AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO. 

Mimi ni Mathayo daudi sudai  karibu tujifunze habari za unafki ambao Mungu haupendi.

Maana inayojulikana ya Unafiki ni ile hali ya kutoa maneno, au kuonyesha hisia au vitendo kwa nje tu, ambavyo kiuhalisia ndani ya mtu huyo havipo.


Kwamfano mtu anaweza kuwa anakuchukia, lakini kwa nje akawa anaonyesha kama kukujali na kukuchekea. Huo ndio unafiki.


Pengine unaweza ukawa unafahamu aina hiyo moja ya unafiki, lakini Leo tutaona aina mbalimbali za unafiki ambazo zinazungumziwa kwenye biblia, na namna gani ya kuzikwepa, kwasababu moja ya dhambi ambazo zinamchukiza Mungu sana ni unafiki, na inawapeleka watu wengi kuzimu pasipo wao kujua.


 1. Aina ya kwanza ni pale unapoijua elimu ya dunia hii kuliko elimu ya Mungu. 


Hilo Bwana Yesu aliliweka wazi kabisa akasema..


Luka 12:54-56 

''54 Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?


Ikiwa Geografia ipo kichwani, kanuni za fizikia umezitunza mpaka unafahamu ni kwanini jani linaanguka chini na haliendi juu, unajua ukiumwa unaweza kwenda kutumia mwarobaini ukapona..Lakini unashindwa kujua kwa Mungu yupo, au hizi ni siku za mwisho. Ukweli ni kwamba Mungu anakuona kama ni mnafiki, na mwisho ukifika hatahangaika kukupa neema ya kumtambua bali utaishia kupotea kwasababu anajua wewe unajiweza, lakini hutaki tu.


  2. Ni pale unapoona matatizo ya wengine sana, kuliko matatizo yako mwenyewe ;

Bwana alisema;

Mathayo 7:3-5

 “3 Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?

4 Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe?

5 Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako”.


Hali hii inakufanya, uwaone wengine wote ni wakosaji, au hawastahili, na matokeo yake Mungu anakuona na kukuhukumu vilevile kama unavyowahukumu wao, Soma habari ya Yule farisayo aliyejihesabia haki zaidi ya mtoza ushuri( Luka 18:9-14) utalithibitisha hilo. Hivyo, hatuna budi, kujiuhubiria kwanza sisi, ndio tuende na kwa wengine.


3. Pale unaposali au unapotoa sadaka, lengo lako likiwa ni utazamwe na watu, kuwa wewe ni mtoaji au mwombaji mzuri, huo Bwana anauona pia kama ni unafiki. 


Alisema:


Mathayo 6:1-2

 “1Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.

2 Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu”.


4. Pale unapoufahamu ukweli lakini unawazuia wengine wasiujue ukweli huo kwa makusudi. 

Mathayo 23:13 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.”


Hii inawahusu sana sana viongozi wa dini, kwamfano pengine wanajua ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa katika maji mengi, lakini hawawafundishi kondoo wao hilo, wanajua, hizi ni siku za mwisho na Yesu yupo mlangoni kurudi, kwamba watu waache dhambi wamgeukie Mungu, kinyume chake wanawahubiria mafanikio tu miaka yote, ili tu wapate fedha. Huo Bwana anauona kama ni unafiki, mbaya sana, na adhabu yake ni ziwa la moto.


5. Unafiki ni pamoja, na kujifanya msafi lakini, ndani ni mchafu :


 Mathayo 23:27-28

“27 Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.

28 Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”.


Hili bado lipo kwa viongozi wa imani, unakuwa askofu au mchungaji, unavaa kanzu nyeupe, unaitwa baba, lakini unafumaniwa na skendo za uzinzi,  unakunywa pombe kichini chini, unapenda mambo ya ulimwenguni. Kwa Bwana ni heri tujionyeshe kuwa sisi ni wakosaji, kuliko kujificha nyuma ya kivuli cha utakatifu ni hatari sana.


6. Unafiki ni pale unapojua unapaswa umtumikie Mungu, lakini hufanyi hivyo kwa kutoa udhuru: 


Soma Mathayo 24:45-51, utaona anazungumzia habari ya Yule mtumwa mwaminifu, ambaye alifanya vyote alivyoagizwa na Bwana wake bila udhuru, lakini mwingine, akajisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia akaanza kuwapiga wafanyakazi wake. Bwana Yesu anasema atakaporudi, atamweka fungu lake pamoja na wanafiki. Epuka udhuru na uvivu katika kumtumikia Mungu.


Mathayo 24:50-51

 “50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua,

51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.


7. Na mwisho, unafiki ni pale unaposisitizia watu wayatimize yale maagizo, madogo, lakini yale ya msingi, na yenye kuokoa, huna habari nayo. 


Kwamfano kuhimiza sana utoaji wa sadaka, ambao kimsingi Bwana mwenyewe alisema tufanye hivyo, lakini pale inapokuwa imezidi kila ibada ni sadaka tu, sadaka tu, mpaka ya mchicha, na tunasahau mambo makuu kama Utakatifu, kumcha Mungu na upendo. Huo ni unafiki mkubwa kwa Bwana..


Mathayo 23:23-24 

 “23 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.

24 Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia”.


Bwana atusaidie tujiepusha na hizo aina saba (7) za unafiki, kwasababu zitatupelekea jehanamu ikiwa zipo ndani yetu.


Lakini swali ni Je! Tunazikwepaje? Jibu ni kwa kumaanisha kumfuata Yesu kwa mioyo yetu yetu.  Kwa jinsi tunavyomkaribia yeye ndivyo anavyotukaribia na sisi, kutusaidia kuwa kama yeye. Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kutoka katika moyo wako, kisha nenda kabatizwe ikiwa hukufanya hivyo, kumbuka ubatizo sahihi ni kwa jina la YESU KRISTO sawasawa (Matendo 2:38). Kisha Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu, ikiwa utapenda upate msaada huo wa wokovu, basi wasiliana nasi kwa namba zinazoonekana chini;


Bwana akubariki.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JE NI DHAMBI KUSHEREHEKEA VALENTINE'S DAY?

MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU

BWANA TUONGEZEE IMANI