DANIELI 10
Nini maana ya kuutia moyo ufahamu? (Danieli 10:12)
SWALI: Nini maana ya kuutia moyo ufahamu? Mtu anatiaje moyo wake ufahamu?
Danieli 10:12 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako”.
JIBU: Ukisoma kitabu cha Danieli chote utagundua Danieli alikuwa ni mtu ambaye si wa kuchulia mambo juu juu tu..alikuwa ni mtu anayechunguza na kufuatilia mambo baada ya kusikia
Kwa mfano angalia ile ndoto aliyoota Nebukadreza..ndoto ile hakuota Danieli, lakini baadaye alipoona ina maana kubwa alimwomba Mungu ampe kujua zaidi..Na ndio hapo utaona Danieli akifuniliwa kwa undani mkubwa sana mambo yahusianayo na ile ndoto, Juu ya zile Milki nne za ulimwengu. Soma Danieli 2,5,7
Ukisoma tena Danieli sura ya 9 utaona..alipokuwa anasoma vitabu akagundua kuwa kumbe imeshaandikwa na nabii Yeremia kuwa Israeli watakaa Babeli kwa muda wa miaka 70 tu..Hilo jambo lilimshangaza kwasababu hakuwahi kudhani kama Israeli ingekaa utumwani kwa muda mfupi vile. Hivyo hakukaa hivyo hivyo tu..Ndipo akaanza kumlilia Mungu kwa toba..baadaye Mungu akamfunilia jinsi itakavyokuwa mpaka mwisho.
Vivyo hivyo kuna wakati mwingine mbeleni biblia inatuambia Danieli alifunuliwa jambo lingine jipya..japokuwa jambo hilo halijaandikwa katika biblia ni lipi…lakini linaonekana lilikuwa ni la kutisha na ndio maana alisema ni vita vikubwa..Sasa alipofuniliwa kwa muhtasari tu,, kama kawaida yake hakukaa tu hivi hivi..bali aliingia katika maombi ya mfungo na maombolezo kwa muda wa wiki tatu nzima kumsihi Mungu amfunulie..
Tusome..
Danieli 10:1-3,
[1]Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo.
[2]Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.
[3]Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia”.
Unaona…Sasa tukiendelea kusoma mbeleni ndio tunaona akitokewa na yule malaika. Na kumwambia maneno haya;
Danieli 10:12
[12]Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.
Kumbe kitendo cha Danieli kuzingatia jumbe alizopewa..mbinguni alikuwa anaonekana kama mtu aliyetia moyo wake ufahamu ili kutaka kujua.
Ni nini tunajifunza kwa Danieli?
Hata sasa, Mungu anatafuta watu kama hawa. Ni mara ngapi watu wanamsikia Mungu akizungumza nao kwa njia mbalimbali hususa kwa Neno lake lakini hawataki kutia mioyo yao ufahamu kusikia?.
Na ndio hapo utashangaa mtu anaona kila kitu ni sawa tu. Hajui kuwa ni Mungu anataka kumpigisha hatua nyingine..lakini yeye anaenda kwa desturi na mazoea ..kila siku kanisani ni kusikia tu Neno basi hatii moyo wake ufahamu wa kutaka kusikia sauti ya Mungu inamwambia nini nyuma yake(Maana yake kuwa hatilii maanani).
Na ndio maana hakuna badiliko lolote la maisha yake.
Mungu huwa anataka tutie mioyo yetu ufahamu kwanza ndipo aseme na sisi zaidi au kutuhudumia, kama alivyokuwa akifanya Danieli.
Shalom
Maoni
Chapisha Maoni